Msumbiji inakabaliwa na vurugu baada ya uchaguzi wa Oktoba 9, 2024./Picha: Reuters  

Idadi ya watu waliopoteza maisha kufuatia vurugu za baada ya uchaguzi nchini Msumbiji sasa imefikia 27, kufuatiwa kuuwawa kwa waandamanaji watatu siku ya Alhamisi, maofisa wa afya nchini humo wamesema.

Hayo yanajiri huku mamlaka nchini humo, ikipeleka askari kwenye maeneo mbalimbali kudhibiti hali ya usalama nchini humo.

Kwa mujibu wa Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Msumbiji, Jenerali Omar Msaranga jeshi hilo lipo tayari kuwasaidia polisi kurejesha utulivu nchiini Msumbiji.

Maandamano yenye vurugu

Miji mingi nchini Msumbiji imeghubikwa na vurugu na maandamano ya mara kwa mara, toka Tume ya Uchaguzi nchini humo (CNE) kumtangaza Daniel Chapo kutoka chama cha Frelimo kama mshindi wa kiti cha Urais dhidi ya Venancio Mondlane kutoka chama cha upinzani.

Chama cha Frelimo kimekuwepo madarakani toka nchi hiyo ilipopata uhuru wake kutoka kwa Wareno, mwaka 1975.

Tuhuma za wizi wa kura

Vyama vya upinzani vimekituhumu chama cha Frelimo kwa udanganyifu kwenye uchaguzi wa Oktoba 9, huku wasimamizi wa kimataifa wakitilia dosari mchakato huo.

Chama cha Frelimo kimekuwa kikituhumiwa kwa wizi wa kura nchini humo. Hata hivyo, Baraza la Katiba la nchi hiyo, bado halijaidhinisha matokeo ya uchaguzi huo kama inavyopaswa kufanyika.

TRT Afrika