Kampeni zimeanza nchini Msumbiji siku ya Jumamosi, ikiwa ni wiki sita kabla nchi hiyo haijafanya uchaguzi wake mkuu.
Wapiga kura wa nchi hiyo watamchagua Rais, wabunge na viongozi wengine katika mchakato uliopangwa kufanyika Oktoba 9, huku Rais Filipe Nyusi mwenye miaka 69 akikosa sifa za kugombea kwa muhula mwingine.
Chama tawala cha Frelimo kimekuwa kikishinda uchaguzi tangu kumalizika kwa vita vyake na Renamo, ambacho ni chama kikuu cha upinzani. Frelimo inaongoza maeneo mengi ya kiutawala.
Chama cha Frelimo kimempitisha Daniel Chapo, mwenye umri wa miaka 47, ambaye atachuana na Ossufo Momade wa Renamo.
Mchuano mkali
Wagombea wengine wawili wa nafasi ya Urais ni pamoja na Lutero Simango kutoka chama cha Democratic na kada wa zamani wa Renamo, Venancio Mondlane ambaye anasimama kama mgombea huru.
Rais wa Tume ya Uchaguzi ya Msumbiji ametaka kuwepo amani wakati wa kampeni, akiwaasa wagombea kuepuka kauli cha chuki.
"Ni lazima tuepuke vurugu za aina yoyote ile kwasabu wagombea wote ndugu zetu licha ya upinzani wa kisiasa," alisema Matsinhe, ambaye pia ni Askofu wa Kanisa la Kianglikana.
Madai ya uchakachuaji
Renamo iliitisha maandamano baada ya Frelimo kutangazwa mshindi wa maeneo ya kiutawala na 64 kati ya 65, ikisisitiza kuwa ilishinda katika mji mkuu, Maputo.
Chama hicho hakijawahi kushinda uchaguzi wowote tangu kumalizika kwa vita vya kupigania uhuru kutoka kwa Ureno mwaka 1975.
Tume ya uchaguzi ya nchi hiyo iliidhinisha majina ya wagombea kutoka vyama 35 vya siasa wanaowania nafasi za ubunge and vyama 14 zinazogombea nafasi za serikali za mitaa.
Nchi ya Msumbiji ilishuhudia vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyohusisha wafuasi wa Renamo na Frelimo kutoka mwaka 1977 hadi 1992, ambavyo pia viliharibu uchumi wa nchi hiyo na kuua watu takribani milioni moja.
Nchi hiyo inashika nafasi ya saba kutoka chini kwenye takwimu ya Maendeleo ya Binadamu yenye mataifa 191 iliyoandaliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa.