Takriban Watutsi 800,000 na Wahutu wenye msimamo wa wastani waliuawa nchini Rwanda mwaka 1994 wakati wa umwagaji damu wa siku 100 | Picha: AA

"Tunashukuru Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa IRMCT ambayo ilifanya kazi na Mwendesha Mashtaka wa Rwanda na mamlaka ya Afrika Kusini kuhakikisha kwamba mtoro mtoro wa mauaji ya halaiki Fulgence Kayishema hatimaye atakabiliwa na haki." Asema Msemaji wa Serikali ya Rwanda, Yolande Makolo katika mahojiano na TRT Afrika leo jioni tarehe 27 Mei.

Fulgence Kayishema, mmoja wa washukiwa waliokuwa wakisakwa zaidi katika mauaji ya halaiki ya Rwanda mwaka 1994, alifikishwa Ijumaa mbele ya mahakama nchini Afrika Kusini.

Kayishema alifikishwa kwa muda katika mahakama ya CapeTown kabla ya kesi yake kuahirishwa hadi Juni 2. Afisa huyo wa zamani wa polisi wa Rwanda, mwenye umri wa miaka 62, alikamatwa Jumatano huko Paarl, mji wa Jimbo la Western Cape nchini Afrika Kusini, baada ya kutoroka kwa miaka 22.

Anatuhumiwa kupanga mauaji ya takriban wakimbizi 2,000 wa Kitutsi katika Kanisa Katoliki la Nyange wakati wa mauaji ya kimbari ya 1994 dhidi ya Watutsi nchini Rwanda

Takriban Watutsi 800,000 na Wahutu wenye msimamo wa wastani waliuawa nchini Rwanda mwaka 1994 wakati wa umwagaji damu wa siku 100.

Kayishema alikamatwa katika operesheni ya pamoja ya mamlaka ya Afrika Kusini na timu ya wafuatiliaji waliotoroka ya International Residual Mechanism for Criminal Tribunals (IRMCT), kulingana na taarifa iliyotolewa na mahakama hiyo maalum ya Umoja wa Mataifa siku ya Alhamisi.

Msemaji wa Serikali ya Rwanda, Makolo amesema kuwa "Takriban miaka 30 baadaye, tuna orodha ndefu ya wakimbizi wa Rwanda waliokimbia mauaji ya halaiki ambao bado wako katika mataifa kadhaa duniani, na tutaendelea kushirikiana na nchi washirika na taasisi kuhakikisha kwamba wanawajibishwa kwa uhalifu uliotekelezwa katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 dhidi ya Watutsi."

Mwendesha mashtaka mkuu wa IRMCT Serge Brammertz alisema Kayishema alikuwa mtoro kwa zaidi ya miaka 20 na "kukamatwa kwake kunahakikisha kwamba hatimaye atakabiliwa na haki kwa makosa yake ya uhalifu."

IRMCT ilisema mauaji ya halaiki ni uhalifu mkubwa zaidi unaojulikana kwa wanadamu na jumuiya ya kimataifa imejitolea kuhakikisha kuwa wahusika wake watachukuliwa hatua na kuadhibiwa.

"Kukamatwa huku ni dhihirisho dhahiri kwamba ahadi hii haififii na kwamba haki itatendeka, haijalishi itachukua muda gani," ilisema taarifa hiyo.

Umoja wa Mataifa siku ya Alhamisi ulikaribisha kukamatwa kwa Kayishema, ukisema: "Kushikwa kwa Bw. Kayishema kunatoa ujumbe mzito kwamba wale wanaodaiwa kufanya uhalifu huo hawawezi kukwepa haki na hatimaye watawajibishwa, hata zaidi ya robo karne baadaye. ," Stephane Dujarric, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, alisema katika taarifa.

Baada ya mauaji ya Nyange, kuwaua wakimbizi wa Kitutsi makanisani ikawa kitu cha kawaida cha mauaji ya kimbari.

AA