Nyong'o, babake mwigizaji maarufu Lupita Nyong'o/ Picha: Anyang' Nyong'o

Gavana wa jiji la Kisumu nchini Kenya ambaye pia ni mshauri wa Umoja wa Mataifa kuhusu serikali za mitaa na mikoa, Profesa Anyang' Nyong'o, ameshutumu vikali uvamizi wa Israel huko Gaza.

Nyong'o, babake mwigizaji maarufu wa filamu Lupita Nyong'o, ameyataka mataifa ya Afrika kukata uhusiano wa kidiplomasia na Israeli kuonyesha mshikamano na Wapalestina.

"Mzozo wa umwagaji damu kati ya Israeli na Palestina umekuwa na athari kubwa kwa nchi nyingi ulimwenguni," Nyong'o aliandika kwenye taarifa rasmi Jumanne.

"Vikosi vya maendeleo barani Afrika, vinavyoongozwa na Umoja wa Afrika, haviwezi kusimama na kuruhusu hili kutokea," Nyong'o alisema.

"Tungependa kukata rufaa kwa Umoja wa Afrika kutoa wito kwa serikali zake zote wanachama, ili kuvunja mara moja, uhusiano wa kidiplomasia na Israeli kama mshikamano na wenzetu huko Gaza na Ukingo wa Magharibi," amesema.

Anyang ' Nyong'o, ambaye pia ni waziri wa zamani wa mipango na maendeleo ya kitaifa, nchini Kenya, ameilaumu Israel kwa mipango yake ya kuvamia Gaza na Ukingo wa Magharibi huku akitaja kuwa italeta athari zaidi kwa hali ya kibanadamau inayoshuhudiwa.

"Sasa ni wazi kwamba Israeli, dhidi ya maslahi ya wahusika wote wa maendeleo katika ulimwengu wa Kiarabu na Israeli mwenyewe, inapanga uvamizi mkubwa wa umwagaji damu Gaza na Ukingo wa Magharibi," amesema Nyong'o.

Septemba mwaka huu, Profesa Anyang' Nyong'o aliteuliwa kuwa mshauri wa Umoja wa Mataifa kuhusu serikali za mitaa na mikoa, na mwanachama wa kundi la ushauri katika kuendeleza miradi ya serikali za mitaa na kikanda.

TRT Afrika