Viongozi katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, wamelaani hujuma ya Israel huko Gaza siku ya Jumamosi na kutaka ukomeshwe mara moja.
Moussa Faki, mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, alisema mashambulizi ya Israel ni ukiukaji "wazi zaidi" wa sheria za kimataifa za kibinadamu na kuishutumu Israel kwa "kuwaangamiza" wakaazi wa Gaza.
Faki alizungumza pamoja na Waziri Mkuu wa Palestina Mohammad Shtayyeh, ambaye pia alihutubia mkutano huo.
"Uwe na hakika, tunalaani vikali mashambulizi haya ambayo hayajawahi kutokea katika historia ya wanadamu," Faki alisema huku akishangiliwa na wajumbe. "Tunataka kukuhakikishia mshikamano wetu na watu wa Palestina."
'Mauaji ya kimbari mbele ya kadamnasi'
Azali Assoumani, rais wa Comoro na mwenyekiti anayeondoka wa Umoja wa Afrika, alipongeza kesi iliyowasilishwa na Afrika Kusini dhidi ya Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki huku akilaani "mauaji ya halaiki inayofanywa na Israel huko Palestina chini ya pua zetu."
"Jumuiya ya kimataifa haiwezi kufumbia macho ukatili unaofanywa ambao sio tu umezua machafuko nchini Palestina lakini pia umekuwa na matokeo mabaya katika dunia nzima," Assoumani alisema.
Mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza yamesababisha vifo vya takriban Wapalestina 29,000 wengi wao wakiwa wanawake na watoto. Lakini inakanusha kufanya mauaji ya kimbari.
Wakati wa mkutano wa kilele wa AU mwaka jana, mjumbe wa Israel aliondolewa kwenye ukumbi wa kikao huku kukiwa na mzozo kuhusu hali ya waangalizi wa nchi hiyo katika baraza la bara hilo.