Mke wa mwanasiasia wa upinzani nchini Uganda aliyezuiliwa Kizza Besigye alisema Jumapili "ana wasiwasi sana" kuhusu afya yake, karibu wiki moja baada ya mgombea huyo wa zamani wa urais kuanza mgomo wa kutokula.
Besigye, 68, ni mpinzani mkuu wa Rais wa nchi hiyo Yoweri Museveni - aliye madarakani kwa karibu miaka 40 - ambaye amempinga bila mafanikio katika uchaguzi mara nne.
Katika kesi ya "kutishia usalama wa taifa", Besigye aligoma kula mnamo Februari 10 kupinga kuzuiliwa kwake, huku wakili wake akimtaja kuwa "mgonjwa sana."
"Hajakula, anakunywa maji tu," mkewe, mkurugenzi mtendaji wa UNAIDS, Winnie Byanyima, aliiambia AFP siku ya Jumapili kando kando ya mkutano wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa.
'Mnyonge na amepungukiwa maji'
"Anasema ni kitendo chake pekee cha kupinga kuwekwa kizuizini kinyume cha sheria."
Wakati Besigye alipoonekana hadharani mara ya mwisho, wakati wa kufikishwa mahakamani siku ya Ijumaa, "alionekana dhaifu sana na kukosa maji mwilini," alisema.
Aliongeza kuwa "ana wasiwasi sana kuhusu hali yake sasa."
Besigye alitekwa nchini Kenya mwezi Novemba, na amekuwa akikabiliwa na kesi ya uhaini ambayo hukumu yake ni kifo katika mahakama ya kijeshi.
'Kupigania haki'
Museveni alikataa uamuzi wa mwezi uliopita wa mahakama ya juu kwamba raia wasihukumiwe katika mahakama za kijeshi.
Hapo awali Byanyima aliitaja kesi hiyo kuwa "uzushi".
"Niko katika kupigania haki," aliiambia AFP.
"Ikiwa hii itatokea kwake, kwamba anaendelea kuzuiliwa kinyume cha sheria, kwamba mchakato wa uwongo unatumiwa kumtia hatiani, hii sio kwa ajili yake tu, ni kuhusu hatima ya demokrasia na haki za Waganda," alisema.
Umoja wa Mataifa na mashirika kadhaa ya kutetea haki za binadamu yameelezea wasiwasi wao kuhusu kukandamizwa kwa upinzani wa kisiasa nchini Uganda katika maandalizi ya uchaguzi wa rais wa 2026.
Kundi la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeitaja kesi ya Besigye kuwa "ukiukaji wa haki."