Na Mwandishi Wetu
Ufunguzi wa Michuano hii mikubwa kupata kutokea barani Afrika ulifanyika Januari 13, katika uwanja wa Alassane Ouattara, katika mji wa kibiashara wa Abidjan.
Michuano hiyo itadumu mpaka tarehe 11, mwezi wa pili wakati mshindi atakabidhiwa kombe lake pamoja na kitita cha dola za Kimarekani 7,000,000.
Hii ni mara ya kwanza kwa nchi hiyo kutoka Afrika Magharibi kuandaa mashindano hayo toka ilivyofanya hivyo mwaka 1984.
Kiasi cha dola za kimarekani bilioni 1.5 zimetengwa na serikali ya Ivory Coast kama sehemu ya kuboresha miundombinu na maandalizi mengine ya mashindnao hayo makubwa barani Afrika.
Michuano hiyo itarindima kwenye viwanja sita ndani ya miji mitano nchini Ivory Coast.
Pamoja na burudani ya kukata na shoka ya kabumbu kutoka wachezaji mahiri barani Afrika, mila, tamaduni na desturi kutoka nchi 24 zitatia nakshi michuano hiyo.
Ikiwa imeanzishwa mwaka 1957, michuano ya AFCON imekuwa na utofauti wa kipekee, wakati wa maandalizi yake.
Mechi ya kufungua dimba, iliwakutanisha Ivory Coast dhidi ya Guinea-Bissau, huku wenyeji wakiibuka na ushindi wa magoli mawili kwa bila.
Michuano hii ilipangwa kufanyika Juni na Julai mwaka jana ili kuepusha mgongano na misimu ya katikati kwenye ligi nyingi za Ulaya ambazo wachezaji wengi kutoka Afrika wanahudumu.
Hata hivyo, hilo halikutokea baada ya mvua kubwa kunyesha nchini Ivory Coast, jambo lililopelekea michuano hiyo kupelekwa mbele mpaka Januari na Februari 2024.