Mawaziri nchini Kenya wamesaini mikataba ya utendaji chini ya usimamizi wa rais William Ruto ili kutimiza matarajio na matakwa ya serikali yake.
Mawaziri hao kutoka wizara mbalimbali, walishiriki katika hafla ya kutia sahihi mkataba wa huo wa kipindi cha mwaka mmoja katika ikulu ya rais jijini Nairobi kama hatua ya kufanikisha malengo na mipango ya serikali hiyo.
Rais Ruto amewaonya vikali mawaziri wake dhidi ya ufisadi huku akieleza kuwa hatoruhusu utendaji wa serikali kulemazwa na tamaa za kibinafsi.
"Hatutosubiri hadi pesa za umma zipotee. Hakuna pesa za kuiba. Pesa tulizonazo ni za miradi ya maendeleo kutimiza ndoto za wakenya. Hatutasubiri kuona pesa zikipotea. Pindi tu, tutakapogundua una nia ya wizi wa fedha, utachukuliwa hatua." Alieleza.
"Mkataba huu mnaosaini leo, ni hatua mojawapo za kuwawajibikia wananchi na kutimiza ahadi nilizofanya nao. Aidha, mkataba huu wa utendaji utahakikisha utekelezaji wa shughuli na mipango ya serikali kulingana na ruwaza ya utawala wangu"
Rais huyo alionekana kusikitishwa na hatua ya baadhi ya mawaziri wake kuchelewa kufika katika hafla hiyo, huku akiongeza kuwa kuzingatia muda ipasavyo ni katika kuheshimu mkataba wa utendaji na utoaji huduma.
"Kuna baadhi ya mawaziri hapa waliochelewa kufika katika hafla hii. Ni lazima kila mmoja afafanue kupitia kuandika sababu za kutofika kulingana na wakati." Rais aliongeza.
Kiongozi huyo wa awamu ya tano amelaani matumizi ya nguvu na polisi pamoja na vurugu za hivi majuzi vilviyoshuhudiwa nchini humo.
"Hatujakabiliana na mauaji ya visa vya mauaji ya kiholela mikononi mwa polisi ili tutowe fursa kwa marudio ya matukio kama hayo. Tunalaani vitendo vya fujo na vurugu. Hatukubali matumizi ya ghasia na wanasiasa wa sasa na wa zamani kwenye siasa kwani inapelekea vifo vya watu. Tunapinga matumizi ya ghasia kwenye siasa." Rais Ruto alisema.
Mkataba wangu wa utendaji unaweka malengo ambayo serikali lazima ifanikishe, katika kumlisha kila Mkenya, kutoa nyumba za bei nafuu kote nchini, kutimiza afya kwa wote, kuanzisha miundombinu muhimu kwa ajili ya ukuaji wa kasi wa uchumi wa kidijitali na ubunifu, pamoja na kutengeneza mamilioni ya ajira kwa wakenya.
Kwa upande wake, Naibu wa Rais Rigathi Gachagua ametilia mkazo marufuku ya ziara za ngambo kwa maafisa wakuu wa serikali wakiongozwa na mawaziri. Ameongeza kuwa marufuku hiyo itaimarisha utendaji kazi kwani kutokuwepo kwa baadhi ya mawaziri na makatibu imelemaza utoaji huduma muhimu.