Rapa AKA aliuawa kwa kupigwa risasi mjini Durban tarehe kumi mwezi Februari mwaka huu. Picha: Getty

Kamishna wa polisi wa KwaZulu-Natal, Luteni Jenerali Nhlanhla Mkwanazi ametangaza siku ya Jumatano kuwa wamefanikiwa kupata silaha iliyotumika kumuua rapa Kiernan Forbes, maarufu kwa jina la AKA.

Kamishna huyo ameyasema hayo akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari ulioandaliwa na kamati ya mawaziri kuhusu mauaji ya kisiasa katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Durban.

Rapa Kiernan Forbes anayejulikana kama 'AKA', na rafiki yake Tebello Tibz Motsoane waliuawa kwa kupigwa risasi mjini Durban tarehe 10 mwezi Februari.

AKA kutoka Afrika Kusini, amepata umaarufu Afrika mashariki kwa Collabo yake na Diamond Platnumz kwa 'Make Me sing'. Picha: Getty

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye mkutano wa Kamati ya Mawaziri kuhusu mauaji ya kisiasa katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Durban, Mkwanazi alisema wamebaini kuwa baadhi ya magari yaliyotumika katika mauaji hayo.

"Tumetambua angalau bunduki moja iliyotumiwa na tumebaini kuwa ilimpiga risasi na kumuua Forbes (AKA)," alisema Mkwanazi.

"Tumetambua pia angalau magari kadhaa ambayo yalitumika. Baadhi ya magari yalitumika kutoroka eneo la mauaji. Ni magari ambayo huenda yalitumiwa na watu hawa ambao ni washukiwa wa tukio hili." Aliongeza.

Mkwanazi ameongeza kuwa wanaendelea na mazungumzo na Mamlaka ya Mashtaka ya Taifa (NPA) ili kubaini baadhi ya watuhumiwa.

TRT Afrika