Mji mkuu wa Sudan Khartoum umeripotiwa kuongezeka mapigano katika maeneo kadhaa siku ya Jumapili baada ya kumalizika kwa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya makundi hasimu ya kijeshi yanayo simamiwa na Saudi Arabia na Marekani, shirika la habari la Reuters linaripoti.
Kulingana na mashahidi, ndege ya kijeshi ilianguka huko Omdurman, moja ya miji mitatu karibu na Nile ambayo inaunda eneo kubwa la mji mkuu.
Jeshi bado halijatoa tamko kufuatia ongezeko ambalo limewafanya watumie ndege za kivita kuwalenga wanajeshi wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) kilichoenea katika mji mkuu.
Saudi Arabia na Marekani zilisema bado kuna mazungumzo yanayoendelea kati ya jeshi na RSF, ambayo yamesalia Jeddah ingawa mazungumzo ya kurefusha usitishaji mapigano yalisitishwa wiki iliyopita.
"Majadiliano hayo yanalenga kuwezesha usaidizi wa kibinadamu na kufikia makubaliano juu ya hatua za karibu ambazo pande zote lazima zichukue kabla ya mazungumzo ya Jeddah kuanza tena," nchi hizo mbili zilisema katika taarifa ya pamoja.
Makubaliano ya kusitisha mapigano yalianza Mei 22 na kumalizika Jumamosi jioni. Ilikuwa imesababisha kupungua kwa kasi ya mapigano na ufikiaji mdogo wa kibinadamu, lakini kama mikataba ya awali ya makubaliano, ilikiukwa mara kwa mara.
Miongoni mwa maeneo ambayo mapigano yaliripotiwa siku ya Jumapili ni kati na kusini mwa Khartoum, na Bahri, ng'ambo ya Blue Nile kuelekea kaskazini.
Mgogoro wa wiki saba wa udhibiti wa nchi kati ya jeshi na RSF umewafanya watu wapatao milioni 1.2 kuwa wakimbizi ndani ya nchi hiyo na kusababisha wengine 400,000 kukimbilia nchi jirani.