Idara ya Hazina ya Marekani siku ya Jumatatu ilitangaza vikwazo kwa kile ilichosema ni mtandao wa kimataifa wa kukusanya na utakatishaji fedha kwa niaba ya kundi la wanamgambo wa al Shabaab linaloendesha shughuli zake nchini Somalia.
Vikwazo hivyo vililenga mashirika 16 na watu binafsi kote katika eneo la Pembe ya Afrika, Umoja wa Falme za Kiarabu na Cyprus, Hazina ilisema katika taarifa yake.
''Watu binafsi ndani ya mtandao huu ni pamoja na wafanyabiashara wenye ushawishi mkubwa katika eneo hilo ambao hutoa msaada wa kifedha kwa al-Shabaab, kikundi cha kigaidi kilichohusika na baadhi ya mashambulizi mabaya zaidi ya kigaidi katika historia ya kisasa ya Afrika Mashariki,'' ilisema taarifa katika mtandao wa Idara hiyo.
Miongoni mwa biashara zilizoathirika ni Haleel Commodities Limited, inayoendesha shughuli zake kutoka Umoja wa Milki ya Kiarabu UAE, na matawi ndani ya Kenya na Uganda.
Idara ya Marekani imetaja kampuni ya mabasi ya usafiri ya Crown nchini Kenya miongoni mwa biashara zoinazodaiwa kusaidia kufadhili kundi la Al shabaab.
Idara hiyo pia imeelezea katika mtandao wake kuwa ilihusisha mamlaka za Somalia katika kutambua washukiwa wa mtandao huo.
"Hatua ya leo ni sehemu ya juhudi nyingi za idara yetu kuunga mkono kampeni ya hujuma ya kiuchumi ya serikali ya Somalia dhidi ya al-Shabaab-moja ya nguzo tatu katika kampeni yao ya kudhalilisha kundi hili baya la kigaidi," ilisema taarifa hiyo.
Kufuatia hatua hii, mali yote ya watu binafsi au kampuni zinazohiusishwa na biashara zilizotajwa, ambayo ipo Marekani, itafungiwa
Pia tangazo hilo linaharamisha mtu yeyote au mamlaka au biashara ndani ya Marekani kufanya biashara, kujihusisha au kuwasaidia wote waliotajwa kuhusika. Yeyote atakayekutwa na hatia ya kuvunja maagizo haya anatishiwa kukabidhiwa vikwazo vya ziada.
Idara ya usalama aya Marekani inasema kuwa Al-Shabaab huzalisha zaidi ya dola milioni 100 kwa mwaka kwa kuwanyang'anya wafanyabiashara wa ndani na watu binafsi, na pia kupitia usaidizi wa kifedha wa wafanyabiashara washirika.
Somalia imekuwa ikikabiliwa na mashambulio ya mara kwa mara kutoka kwa kundi hilo la Alshabaa wanaodaiwa kuwa nauhusiano na wanamgambo wa Al Qaeda.