Idadi ya vifo vilivyotokana na maporomoko makubwa ya ardhi nchini Papua New Guinea imeongezeka na kufikia zaidi ya 300, mbunge mmoja alisema Jumamosi.
Aimos Akem, mbunge kutoka jimbo la Enga, alisema maporomoko ya ardhi yaliyokumba eneo la Maip-Mulitaka mapema Ijumaa yamebomoa nyumba 1,182 katika eneo la LLG Vijijini, kulingana na PNG Post Courier.
Watu zaidi ya 300 wanahofiwa kuzikwa na maporomoko hayo ambayo pia yameharibu vijiji sita katika eneo hilo.
Maporomoko ya ardhi yaliharibu kijiji cha Yambili katika jimbo la Enga, ambalo ni zaidi ya kilomita 600 kaskazini magharibi mwa mji mkuu Port Moresby.
Mark Ipuia, kiongozi wa eneo hilo alisema kijiji cha Yambali kimefunikwa na mawe makubwa yaliyosababishwa na maporomoko hayo.
Msaada kutoka nje
Mamlaka bado hazijathibitisha idadi ya watu waliofariki.
Maporomoko hayo pia yamefunga barabara inayoelekea katika mji wa Porgera, ambako kuna mgodi mkubwa wa dhahabu.
Kwa nyakati tofauti, Marekani na Australia zimetoa msaada kwa serikali ya Papua New Guinea.
Rais Joe Biden na mkewe walitoa salamu za pole kwa waathirika wa tukio hilo kupitia ujumbe.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia Penny Wong amesema kuwa Canberra iko tayari kutoa msaada.