Sudan

Vikosi vinavyopigana vya Sudan vilikabiliana tena katika mji mkuu wa taifa hilo mapema Ijumaa, huku mashambulizi ya mabomu na makombora yakiripotiwa katika maeneo kadhaa ya mji mkuu Khartoum, licha ya ripoti za awali kuwa Vikosi vya Msaada wa Haraka vya kijeshi [RSF] kukubali kusitishwa kwa mapigano kwa saa 72 kwa misingi ya kibinadamu.

"Usiku wa Eid al-Fitr, maeneo kadhaa ya Khartoum yalishambuliwa kwa mabomu na bado yanakabiliwa na mashambulizi ya makombora na mapigano kati ya wanajeshi na RSF," shirika la habari la AFP lilinukuu Kamati Kuu ya Madaktari wa Sudan ikisema Ijumaa.

Kikosi cha Msaada wa Haraka cha Sudan [RSF] kimekubali kusitisha mapigano kwa saa 72 kwa misingi ya kibinadamu kuanzia saa 6 asubuhi [saa za ndani].

"Maamuzi hayo yanaambatana na Eid al Fitr iliyobarikiwa ... kufungua njia za kibinadamu ili kuwahamisha raia na kuwapa fursa ya kusalimia familia zao," RSF ilisema katika taarifa yake Ijumaa.

Hakukuwa na maoni ya mara moja kutoka kwa jeshi la Sudan kuhusu tangazo la hivi punde la kusitisha mapigano na RSF.

Takriban watu 350 wameuawa katika vita vya kuwania madaraka kati ya viongozi wawili waliokuwa washirika wa serikali kuu ya kijeshi, mkuu wa jeshi Burhan na kiongozi wa RSF Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo.

Mzozo huo umekatiza matumaini ya maendeleo kuelekea demokrasia nchini Sudan.

Maelfu ya raia walimiminika kutoka mjini Khartoum huku milio ya risasi na milipuko ikisikika siku ya Alhamisi.

Umoja wa Mataifa ulikadiria kuwa watu 10,000-20,000 pia wamevuka hadi Chad kukimbia mapigano katika eneo la magharibi la Darfur.

TRT Afrika