EPRA inahofia kutokea janga la kimazingira huku mapipa ya kuifadhi amafuta ardhini yakitishiwa kupasuka kutokana na mafuriko yanayoendelea. :Picha : Reuters 

Mamlaka ya kudhibiti Nishati na petroli nchini Kenya EPRA , imeelezea wasiwasi kuhusu mifumo ya Tangi ya Kuhifadhi Mafuta ya Chini ya Ardhi (UST), ambayo inaweza kuathirika kutokana na mafuriko au vipindi virefu vya mvua kubwa.

Mamlaka hiyo imesema kuwa wamiliki wamagari wanatakiwa kuwa waangalifu ni sehemu zipi wananunua mafuta ya petroli au diesel kutumia katika magari yao.

EPRA imewaagiza wamiliki wa vituo vilivyofurika mafuta kusitisha mara moja shughuli zao ili kuhakikisha usalama wa raia na kudumisha ubora wa bidhaa za petroli.

''"Kituo chochote cha rejareja cha petroli ambacho kimefurika maji kinapaswa kufungwa na kufuatiliwa kwa muda,'' ilisem ataarifa ya EPRA mtandaoni. ''Vituo vya reja reja vinapaswa kutathmini kiwango cha mafuriko, kusafisha uchafu na kuhakikisha ubora wa bidhaa zake kabla ya kuanza tena kazi," taarifa iliendelea kusema.

Hatari kwa mazingira

Mamlaka hiyo imebainisha kuwa uwepo wa maji kwenye matanki ya kuhifadhia maji chini ya ardhi unaathiri ubora wa bidhaa za Petroli jambo ambalo linaweza kusababisha kuharibika kwa magari.

Katik ataarifa hiyo, EPRA imewataka wamiliki wa stesheni hizo kuwa waangalifu kutokana na uwezekano wa mafuta yaliyohifadhiwa kuvuja na kuchafua mazingira.

''Wamiliki wa vituo vya reja reja wanapaswa kutarajia athari yoyote ya kimazingira ya mafuriko na kuchukua hatua zinazofaa ili kukabiliana nayo," ilisema taarifa.

Iliongzea kuwa itatoa ushauri wa kimkakati na utaalamu kwa wahusika ili kuzuia janga lolote na njia za kudhibiti hali iwapo uvujaji utatokea.

Idadi ya vifo kuongezeka

Kenya imepokea idadi kubwa zaidi ya mvua katika miongo kadhaa , ambayo imesababisha mafuriko na uharibifu mkubwa katika sehemu nyingi hasa mji mkuu Nairobi.

Takwimu zinasema takriban watu 200 wanahofiwa kufariki katika mafuriko hayo, ambayo hadi sasa yamesomba mabarabara, majumba na mashamba ya watu, huku makumi wengine hawajulikani waliko.

Serikali ilitangaza mapema wiki hii kutoa shilingi bilioni 70 kuwasaidia wahanga wa mafuriko japo kumeuwa na malalamiko mitandaoni na kutoka kwa waathiriwa juu ya jibu la serikali kudhibiti hali.

Kwa upande wake Rais WIlliam Ruto alitangaza saa 48 kwa wote wanaoishi katika maeneo ya kingi za mito na mabwawa kuhamia sehemu za juu haraka iwezekanavyo huku nchi ikijiandaa kwa maafa zaidi kutokana na tishio la kupasuka mabwawa mengine na mito kuvunja kingo zake.

Shirika la utabiri wa hali hewa pia limetoa tahadhari kuwa hali bado ni hatari kwani mvua kubwa bado inatarajiwa kuendelea kwa siku kadhaa zijazo.

TRT Afrika