Mamlaka nchini Malawi imeanzisha uchunguzi kuhusu chanzo cha moto katika jengo la serikali katika mji mkuu, Lilongwe, ambao uliharibu rekodi muhimu,
Moto huo wa Jumamosi usiku uliteketeza gorofa ya sita na saba ya jengo ambako ofisi ya usajili ya ardhi, kitengo cha kandarasi cha serikali na idara ya mahakama zilipatikana, Waziri wa Habari Moses Kunkuyu alisema katika taarifa.
Karatasi rasmi kuhusu umiliki wa ardhi na uhamishaji ardhi zinahofiwa kuharibiwa, kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya ndani, lakini serikali ilisema rekodi zote katika Wizara ya Ardhi ziliingizwa katika mfumo wa kidijitali.
“Kwa hivyo taifa halipaswi kuwa na wasiwasi kuhusu madai yoyote ya kupoteza taarifa kwa sababu chafu,” Bw Kunkuyu alisema.
Alisema uchunguzi huo unafanywa na polisi wakiungwa mkono na vyombo vingine vya usalama na matokeo yake yatatangazwa hadharani.
Haikuwa mara ya kwanza kwa jengo hilo kushika moto.
Moto sawia ulisha wahi kuzuka mwaka wa 2019. Mjadala kati ya watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini humo uliangazia tuhuma nyingi kuhusu tukio hilo.
Rais Lazarus Chakwera alichaguliwa kwenye jukwaa la kupambana na ufisadi mnamo 2020 lakini amekuwa akipambana na madai ya ufisadi na upendeleo katika serikali yake.
Makamu wake wa Rais Saulos Chilima anakabiliwa na mashtaka ya rushwa kutokana na tuhuma za kupokea pesa ili kutoa kandarasi za serikali lakini mekana kuhusika na kosa lolote.