Mahakama ya Rwanda imekataa rufaa ya kiongozi maarufu wa upinzani ya kufuta hukumu zake za awali, jambo linalomzuia kugombea dhidi ya Rais Paul Kagame katika uchaguzi wa Julai.
Bernard Ntaganda, mwenye umri wa miaka 55, mkosoaji mkubwa wa kiongozi wa Rwanda, aliwasilisha maombi Mahakama Kuu mjini Kigali mnamo Februari akitaka kufuta hukumu za zaidi ya muongo mmoja uliopita.
Ntaganda ni kiongozi wa pili wa upinzani kuzuiwa kugombea katika uchaguzi wa Julai 15 dhidi ya Kagame, ambaye anatarajiwa kushinda muhula wa nne wa miaka madarakani.
Jopo la majaji watatu lilitoa uamuzi dhidi ya Ntaganda, kwa kile walichosema ni kushindwa kwake kulipa ada za mahakama za faranga 106,000 za Rwanda (takriban $82) zinazohusiana na kesi ya awali dhidi yake.
'Sio matokeo ya kushangaza'
"Mahakama Kuu imesema kuwa Ntaganda hakuzingatia sheria zinazowataka watu kuomba hukumu zao zifutwe, na kwa hivyo inakataa rufaa yake," mahakama ilisema Jumanne.
Ntaganda, wakili na mwanzilishi wa chama cha PS-Imberakuri, alisema ana ushahidi kuwa amelipa ada hizo lakini uamuzi wa mahakama "haukuwa matokeo ya kushangaza."
"Chama tawala cha RPF (Rwandan Patriotic Front) hakiwezi kuruhusu mahakama kuwa huru," aliambia AFP.
Ntaganda pia alipanga kugombea dhidi ya Kagame mnamo 2010, lakini alikamatwa kabla ya uchaguzi.
Kifungo cha miaka minne
Alitumikia kifungo cha miaka minne gerezani kwa mashtaka ya kutishia usalama wa taifa na kuchochea mgawanyiko wa kikabila kabla ya kuachiliwa mwaka 2014.
Chini ya sheria za Rwanda, mtu aliyekutwa na hatia na kuhukumiwa kifungo cha zaidi ya miezi sita gerezani anazuiwa kushika nafasi ya umma.
Mwezi Machi, mahakama pia ilikataa kufuta hukumu za awali dhidi ya mpinzani wa Kagame Victoire Ingabire, jambo lililomfanya asiweze kugombea Julai.
Kagame, mwenye umri wa miaka 66, amekuwa kiongozi wa nchi hiyo ndogo isiyo na bandari tangu mauaji ya kimbari ya 1994, rasmi akawa rais mwaka 2000.
Jaribio la urais la Diane Rwigara
Tangu wakati huo ameshinda chaguzi 2003, 2010 na 2017, kila wakati akiwa na zaidi ya 90% ya kura.
Wiki iliyopita, Diane Rwigara, mkosoaji mwingine wa Kagame, alitangaza kuwa anapanga kugombea mwaka huu baada ya kuzuiwa katika uchaguzi wa 2017 kwa madai ya kughushi sahihi za wafuasi kwa ajili ya maombi yake.
Alikamatwa na kushtakiwa kwa kughushi na kuchochea uasi, na alifungwa gerezani kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Watu wengine wawili wamejitokeza kugombea mwaka huu – Frank Habineza wa chama cha Green Party na mgombea huru Philippe Mpayimana.