Felix Tshisekedi alipata zaidi ya 73% ya kura zilizopigwa ili kupata marudio ya uchaguzi wa urais wa Disemba 20, 2023 wa Kongo. / Picha: AFP

Mahakama ya Katiba nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imetupilia mbali maombi mawili yaliyowasilishwa kupinga ushindi wa Rais aliye madarakani Felix Tshisekedi.

Mahakama ilianza kusikiliza maombi hayo Jumatatu, na baada ya siku mbili, ilitoa uamuzi wake, ikisema kwamba maombi hayo hayana uhalali .

Malalamiko hayo yaliwasilishwa tofauti na mgombea urais, Theodore Ngoy, na raia mwingine.

Walalamishi walidai kuwa uchaguzi wa urais wa Desemba 20, 2023, ambao Tshisekedi alitangazwa mshindi kwa kura milioni 13.06 (73.34%), ulikumbwa na dosari.

Katumbi, Fayulu washindwa kuwasilisha malalamiko

Wagombea wa upinzani, wakiongozwa na mshindi wa pili Moise Katumbi, walikataa matokeo ya uchaguzi, kwa madai kuwa uchaguzi uliegemea upande wa Tshisekedi.

Ingawa wagombea wakuu wa upinzani walipinga matokeo hayo, hawakuwasilisha malalamiko katika mahakama ya kikatiba, kwa madai kuwa mahakama hiyo inaunga mkono serikali.

Theodore Ngoy, ambaye alikuwa wa mwisho katika uchaguzi uliovutia wagombeaji 20, aliwasilisha ombi la kutaka ushindi wa rais mteule ubatilishwe.

Ngoy aliiambia mahakama kwamba kulikuwa na "ukiukwaji wa wazi wa sheria ya uchaguzi," akiongeza kuwa "hali ya kijamii na kisiasa nchini, mchakato usio wa kawaida wa uandikishaji wa wapigakura na kuongezwa kwa siku saba kwa mchakato wa kupiga kura" viliongeza dosari ya uchaguzi.

Ombi la kurudiwa uchaguzi

Mlalamishi aliiomba mahakama kubatilisha ushindi wa Tshisekedi, na kuamuru uchaguzi mpya ufanyike baada ya bodi mpya ya uchaguzi kuundwa.

Ombi lake pamoja na lile la mlalamishi mwenzake lilikataliwa Jumanne.

Katumbi alipata 18% ya kura zilizopigwa akimfuata Tshisekedi, huku mshindi wa tatu Martin Fayulu akipata 5% ya kura.

Baadhi ya watu milioni 18 kati ya milioni 44 waliojiandikisha kupiga kura walipiga kura zao katika uchaguzi wa rais wa Kongo, bodi ya uchaguzi ya nchi hiyo, CENI, ilisema.

Uamuzi wa mahakama sasa unafungua njia kwa Tshisekedi kuapishwa kwa muhula wa pili.

TRT Afrika