Uamuzi huo wa mahakama ya juu unaonekana kuwa ushindi kwa sera za Rais William Ruto. Picha / Reuters

Mahakama ya Juu ya Kenya, Jumanne ilibatilisha uamuzi wa mahakama ya rufaa uliozuia sheria ya fedha ya 2023, ushindi wa serikali baada ya maandamano kumlazimisha Rais William Ruto kuondoa mswada wa fedha wa mwaka huu.

Miswada hiyo ya fedha ndiyo njia kuu ya serikali kuweka mikakati ya kuongeza mapato, na utawala wa Ruto umekuwa ukiegemea sheria ya fedha ya 2023 kuendelea kukusanya ushuru baada ya kurejeshwa kwa sheria ya mwaka huu.

"Tunaweka kando uamuzi wa Mahakama ya Rufaa unaotangaza Sheria yote ya Fedha ya 2023 kuwa kinyume na katiba," Mahakama ya Juu ilisema katika uamuzi wake.

Sheria ya 2023 ilipingwa mahakamani kufuatia duru ya maandamano yaliyoongozwa na upinzani mwaka jana, baada ya serikali ya Ruto kuitumia kuongeza maradufu ushuru wa ongezeko la thamani ya mafuta, kuanzisha ushuru wa nyumba na kuongeza kiwango cha juu cha ushuru wa mapato ya kibinafsi, miongoni mwa hatua zingine.

Maandamano makali

Serikali ya Ruto, ambayo ilichukua mamlaka mnamo Septemba 2022, ilitaka kulazimisha awamu mpya ya nyongeza ya ushuru mwaka huu, na kukasirisha raia wengi na kusababisha maandamano mabaya mnamo Juni na Julai ambapo zaidi ya watu 60 waliuawa.

Machafuko hayo yalimlazimu Ruto kuondoa toleo la mwaka huu la sheria ya fedha punde tu baada ya kupitishwa na bunge la kitaifa, na kuchelewesha kuidhinishwa kwa awamu mpya ya ufadhili kutoka kwa Shirika la Fedha la Kimataifa IMF.

Ruto amedai kuwa nyongeza ya ushuru ni muhimu kusaidia kufadhili mipango ya maendeleo nchini Kenya, nchi yenye uchumi mkubwa zaidi Afrika Mashariki, na kulipa deni kubwa la umma.

Mkopo wa IMF

Bodi kuu ya IMF inatazamiwa kukutana ili kuidhinisha malipo hayo mapya Jumatano baada ya Kenya kutimiza malengo iliyoagizwa na Hazina hiyo katika kukagua mpango wake wa mkopo.

Mnamo Julai, Mahakama ya Rufaa ya Kenya ilitangaza sheria ya fedha ya 2023 kuwa kinyume na katiba, lakini mahakama kuu iliahirisha uamuzi huo hadi isikilize rufaa iliyowasilishwa na serikali.

TRT Afrika