Wakiwa wamebeba mabango yenye ujumbe mbalimbali, wakazi wanaoishi ndani ya eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) walifunga barabara inayounganisha hifadhi za Ngorongoro na Serengeti, na hivyo kuathiri shughuli za utalii katika maeneo hayo.
Katika tukio hilo lililotokea asubuhi ya Agosti 18, 2024, muda ambao shughuli za utalii huanza, wanajamii hao walifanya maandamano ya amani, wakilalamikia uonevu unaofanywa na serikali kupitia NCAA, hasa kupitia zoezi la kuhamishwa na kupelekwa kijiji cha Msomera kilichopo mkoa wa Tanga, nchini Tanzania.
Waandamanaji hao pia walipaza sauti dhidi ya serikali ya nchi hiyo, ikiituhumu kwa kukiuka haki zao za ardhi, kunyimwa huduma muhimu za kijamii, kuhamishwa kwa lazima na kupangiwa maeneo mapya ya kupigia kura katika mchakato wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa baadaye mwaka huu.
Mwaka 2021 serikali ya Tanzania ilikuwa imeshaweka mpango wa kuwahamisha takribani watu 82,000 wa jamii ya Kimaasai kutoka katika makazi yao katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.
Serikali ya kikoloni ya Waingereza ilianzisha NCA mwaka 1959, eneo linalotambulika kwa matumizi mseto na kuanzisha makazi ya kudumu ya watu waliokuwa wanaishi ndani na maeneo yanayozunguka bonde la Ngorongoro, wengi wao wakiwa ni wafugaji wa asili ya Kimasai.
Picha mbalimbali za Video zilizosambaa mitandaoni, zilionesha wanajamii hao wakifunga barabara za kuelekea hifadhini, hali iliyowalazimu watalii kuegesha magari yao.
Kwa mujibu wa jamii hiyo maarufu kwa ufugaji nchini Tanzania, NCAA imekuwa ikiwanyanyasa watu hao, ikiwa ni pamoja na kuwanyima huduma muhimu za kijamii.
Kati ya wakazi zaidi ya 100,000 wa eneo la Ngorongoro, ni wakazi wasiozidi 7,500 pekee ndio wamehamishwa kuelekea katika eneo la Msomera lililopo Handeni, Tanga.
"Tunahitaji ardhi yetu," alisema Isaya Ole Pose, mmoja wa waandamanaji.
"Ibara ya 24 ya Katiba inampa kila mtu haki ya kumiliki mali. Ardhi ni mali ambayo kila Mtanzania ana haki ya kumiliki.
Katika ukurasa wake wa X, Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA alionesha kuunga mkono wa jamii hiyo ya Wamaasai katika kudai haki zao.
Hata hivyo, katika taarifa yake, NCAA ilisisitiza kuwa shughuli za kitalii zilikuwa zinaendelea kama kawaida licha ya maandamano hayo.
“Mamlaka inawahakikishia Watalii wote waliopanga safari za kuja Ngorongoro kuwa Serikali itaendelea kusimamia usalama wao wakati wote watakapokuwa ndani ya hifadhi," sehemu ya taarifa hiyo ilisomeka.