Mawimbi mapya ya maandamano yanatarajiwa kutikisa mji mkuu wa Kenya, Nairobi, katika maandamano ya mwezi mzima yanayoongozwa na vijana wa Kenya dhidi ya serikali ya Rais William Ruto siku ya Jumanne tarehe 22 Julai.
Waandamanaji wamejipanga kupitia mitandao ya kijamii ya X pamoja na TikTok na sasa wanapanga kuvuruga shughuli za usafiri wa anga katika uwanja wa ndege mkubwa zaidi Afrika Mashariki, JKIA, jijini Nairobi. Uwanja huo wa ndege hupokea zaidi ya abiria milioni 2.5 kwa mwaka.
Wakenya waliokerwa na uamuzi wa Rais William Ruto wa kuwaajiri tena mawaziri sita wa zamani, walitumia X, ambalo hapo awali lilijulikana kama Twitter, kupanga maandamano chini ya hashtag "OccupyJKIA."
Neno 'Occupy' linatumika nchini Kenya kumaanisha "kukusanyika" mahali fulani.
Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Kenya (KAA) ilisema katika taarifa yake ya Jumatatu: "Kutokana na kuimarishwa kwa ukaguzi wa usalama na taratibu katika JKIA, abiria wanashauriwa kufika uwanjani mapema ili kuepuka ucheleweshaji wowote wa safari zao za ndege. Tafadhali wasiliana na shirika lako la ndege kwa taarifa za hivi punde kuhusu safari za ndege."
Katika barua iliyotumwa kwa wananchi siku ya Jumatatu, polisi wameweka wazi kwamba wanazingatia sheria na kanuni za nchi ambazo zinataka kulindwa kwa maeneo yaliyotambuliwa na sheria za nchi kama hifadhi.
Kile kilichoanza kama maandamano dhidi ya muswada wa fedha unaoungwa mkono na shirika la kimataifa la Fedha, IMF, kimegeuka kuwa suala la kifo na maisha, huku serikali ikituhumiwa na wanaharakati wa kiraia na mashirika ya haki za binadamu nchini Kenya kwa kuua takribani waandamanaji 60 na wengine wengi kupotea au kufungwa katika mahabusu kote nchini.
Angalau miili 10 ilipatikana wiki iliyopita kutoka kwenye machimbo ndani ya Nairobi kufuatia maandamano ya wiki zilizopita ambapo polisi wanatuhumiwa kutumia mbinu za kikatili kudhibiti umati wa waandamanaji wanaoendelea kuongezeka. Wengi wa waandamanaji walipoteza maisha yao baada ya kukutana na polisi mitaani katika miji ya Nairobi, Mombasa, Nakuru, na Kakamega, ambayo ni baadhi ya miji mikubwa katika nchi iliyoathiriwa na mgogoro huo.