Rais Joseph Boakai ameapa kuangalia wasiwasi wa wake za wanajeshi. / Picha: Reuters

Waziri mpya wa ulinzi wa Liberia Jumatatu alijiuzulu kutoka wadhifa wake siku 10 tu baada ya kuteuliwa, kufuatia maandamano ya wake za wanajeshi, ofisi ya rais ilisema.

Kujiuzulu huko kunaashiria mzozo wa kwanza wa kisiasa unaomkabili rais mpya wa Liberia Joseph Boakai tangu kuapishwa kwake mwishoni mwa Januari.

Boakai "amepokea na kukubali barua ya kujiuzulu kutoka kwa Waziri wa Ulinzi wa Kitaifa aliyethibitishwa hivi majuzi Bw. Prince C. Johnson," ofisi ya rais ilisema katika taarifa.

Malalamiko yao

Wake wa wanajeshi wa Liberia waliweka vizuizi vya barabarani karibu na mji mkuu Monrovia na kwingineko nchini, na kumlazimu Boakai kufuta sherehe zilizopangwa za Siku ya Jeshi la Kitaifa siku ya Jumatatu, mwandishi wa AFP aliripoti.

Wanawake hao walikuwa wakitangaza malalamiko mengi kuanzia mishahara duni na pensheni, ukosefu wa hifadhi ya jamii, uhaba wa umeme na ufisadi ndani ya jeshi.

Pia walimtaka waziri wa ulinzi kujiuzulu wakilaumu kupunguzwa kwa mishahara ya wanajeshi wa Liberia wanaorejea kutoka misheni ya amani nchini Mali.

Katika barua yake ya kujiuzulu, Johnson alitaja "machafuko ya sasa ya kisiasa na ya kiraia yaliyosababishwa na maandamano ya wanawake wanaoaminika kuwa wake wa watu wa huduma".

Alitaka "kulinda amani na usalama wa Nchi", taarifa hiyo iliongeza.

Vyombo vya jikoni

Kizuizi cha kwanza kiliwekwa Jumapili kwenye viunga vya Monrovia karibu na kambi ya Edward Binyah Kesselly kwenye barabara inayoelekea uwanja wa ndege wa kimataifa.

Vizuizi vipya vilivyokuwemo vyombo vya jikoni na vifaa vya nyumbani vilionekana mahali pengine nchini siku ya Jumatatu.

Madereva waliokwama kwenye foleni ndefu za magari kwenye barabara inayoelekea uwanja wa ndege waliamua kuyaacha magari yao na kuendelea na safari kwa miguu.

Rais Boakai alilitaka jeshi siku ya Jumatatu kuhakikisha kuwa vizuizi hivyo vimeondolewa "mara moja", kulingana na ofisi ya rais.

Kuchunguza malalamiko hayo

Alikutana na wake za wanajeshi siku ya Jumapili na kuapa kuchunguza kwa makini wasiwasi wao na kuunda tume, timu yake ilisema.

Aliagiza kurejeshwa kwa umeme katika kambi ya Edward Binyah Kesselly na madarasa ya bure katika shule hiyo iliyoko ndani ya kambi.

"Rais amekuwa ofisini kwa siku 20 pekee na amechukua hatua za haraka tayari kushughulikia baadhi ya masuala haya ambayo yamekuwa yakitokota kwa zaidi ya miaka mitano," timu yake ilisema katika taarifa yake.

Boakai "alishauri kila mtu kuwa mtulivu na mwenye amani huku serikali ikitafuta kushughulikia matatizo yao", iliongeza.

TRT Afrika