Kwa 'udi na uvumba' Gambia wanatafuta kuweka historia katika kombe la dunia U-20

Kwa 'udi na uvumba' Gambia wanatafuta kuweka historia katika kombe la dunia U-20

Gambia wanataka kuungana na Nigeria katika jukwaa la robo fainali katika mechi ya kufa au kupona dhidi ya Uruguay
Gambia watakuwa timu ya pili ya Afrika kuingia robo fainali katika mchuano huu wa kombe la dunia U-20 nchini Argentina Picha : Timu ya Gambia 

Miujiza imewafikia timu ya Gambia, na wanatamani waendeleza bahati yao katika mechi ya mchujo ya kombe la dunia ya wachezaji wasiozidi miaka ishirini.

‘‘Kila mmoja yuko tayari kwa mechi hii, na kila mmoja anataka kuweka historia,'' Sainey Sanyang ameambia TRT Afrika.

Mchezaji huyo beki wa Gambia alionesha ujasiri akishikilia jezi yake ya namba tatu mgongoni. Hata hivyo yeye pia anaelewa kibarua kigumu kinachowasubiri. ''Ili tufike fainali, lazima tuzifunge timu kali sana. Tuko tayari hata hivyo,'' aliongeza.

Gambia kufikia sasa wamewashangaza wengi kwa matokeo yao. Wameelea kwa wepesi kupita duru ya makundi waliposhinda mechi yao ya ufunguzi dhidi ya Honduras.

Lakini ushindi wao mkubwa zaidi ni pale walipowalaza vigogo wafaransa 2-1 katika mechi yao ya pili ya makundi, ushindi uliowahakikishia nafasi katika duru ya mchujo na kuwatambulisha kama watu wa kuwaogopa katika mchuano huo.

‘’Unapofanya vyema, watu wanatambua kuwa timu iko sawa na mwisho wa siku sisi tulipokuja tulitazamiwa kuwa wanyonge, ila sasa tumejiinua na kupendwa na wengi,’’ anasema kocha Abdoulie Bojang.

Gambia wanakutana na Honduras huku wakitafuta kupenya robo fainali ya kombe la dunia U-20 Picha AFP

Hata hivyo lazima wawe makini wanapokutana na Uruguay, ambao walifika hapa kwa kuwalaza Iraq na Tunisia.

Akizungumza na TRT Afrika kabla ya mechi Jumatano, kocha Abdoulie anasema ana imani na timu yake.

‘‘Sote tunachukulia mechi kwa umuhimu mkubwa kwani tunataka kuandika historia yetu tukijua kuwa taifa nzima inatuunga mkono.” Anasema kocha Abdoulie.

TRT Afrika