Serikali ya Kenya inataka mashirika yasiyo ya kiserikali kuwa wazi katika shughuli zao. Picha:  Reuters

Na Dayo Yussuf

Mwezi uliopita, serikali ya Kenya ilionya mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo ilisema hayafanyi kazi kwa uwazi na hayazingatii kanuni za nchi.

Katibu Mkuu wa usalama wa ndani na utawala wa kitaifa Raymond Omollo alielezea wasiwasi wake kwamba baadhi ya mashirika haya hayakuwa wazi kuhusu vyanzo vyao vya fedha na rekodi za matumizi.

Omollo ambaye alikuwa akizungumza wakati wa uzinduzi wa Ripoti ya mwaka ya sekta ya mashirika yasiyo ya kiserikali jijini Nairobi alisema alishangazwa na idadi ya mashirika ambayo yalikosa kuwasilisha ripoti zao za kifedha kama inavyotakiwa na sheria.

‘’Hiyo ni sababu tosha ya kudhani kuwa wahalifu wanahusika katika shughuli zisizoeleweka, ikiwa ni pamoja na kufadhili ugaidi,’’ alidai. Hakutaja hadharani NGO yoyote maalum.

Kukiuka sheria

Kwa miaka mingi, kumekuwa na mifarakano ya hapa na pale kati ya serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali ya kigeni na mashirika ya ‘wafadhili’ katika baadhi ya nchi za Afrika.

Baadhi ya NGO, za ndani na kimataifa, bila shaka zina jukumu muhimu katika kusaidia maendeleo ya kijamii na kiuchumi na kisiasa ya nchi.

Baadhi ya NGOs husaidia katika maendeleo ya kiuchumi ikiwa ni pamoja na wafanyabiashara wadogo. Picha: Reuters

Lakini wakati mwingine baadhi yao, hasa zile za nje, wanatuhumiwa kuvuka mipaka yao, kuingilia masuala ya ndani ya nchi wanakfanya kazi na kuendeleza ajenda zinazoendana kinyume na maslahi ya nchi hizo.

Ni kweli kwamba baadhi ya NGO zina hatia linapokuja suala la kutoheshimu sheria za kitaifa, mwenyekiti wa baraza la kitaifa la mashirika yasiyo ya kiserikali la Kenya, Steven Cheboi aliambia TRT Afrika . Baraza la NGO ni chombo-mwavuli cha mashirika yote yasiyo ya kiserikali yaliyosajiliwa nchini.

‘’Tunawahimiza wanachama wetu kuwasilisha marejesho ya kila mwaka. Wanafaa kufichua ufadhili wao kupitia kuwasilisha marejesho ya kila mwaka ili waseme hiki ndicho walichopata na hivi ndivyo walivyotumia,’’ Bw Cheboi aliambia TRT Afrika.

‘’Wasipozingatia, inaeleweka kwamba mtu atawashuku,’’ anaongeza.

Suala la kisiasa

Hata hivyo, Robert Muigai, mwanasheria na mshauri wa haki za binadamu nchini Kenya anasema wakati mwingine baadhi ya maafisa wa serikali hujaribu kushawishi shughuli za NGO kwa manufaa yao hasa kuhusiana na masuala ya kisiasa.

‘’Baadhi ya NGO, hasa zile zinazofanya kazi katika anga za kisiasa, zimekumbwa na muingilio wa serikali hali iliyowalazimu kusimama kwa sauti kubwa,’’ anasema.

Kaskazini mashariki mwa Nigeria, mashirika mengi yasiyo ya kiserikali yanafanya kazi katika masuala ya wahanga wa Boko Haram. Picha: Reuters

Lakini suala hilo si la Kenya pekee. Mwanzoni mwa Machi mwaka huu, serikali ya jimbo la kaskazini-mashariki mwa Nigeria la Adamawa ilisimamisha mashirika yot eyasiyo ya kiserikali - ya ndani na ya kimataifa - ikiyatuhumu baadhi yao kwa kuingilia siasa kabla ya uchaguzi wa ugavana katika jimbo hilo.

"Imegunduliwa kwamba mashirika mengi yasiyo ya kiserikali yamevuka mipaka yao na yanajiingiza katika siasa kwa jina la kutoa msaada wa kibinadamu kwa watu," gavana wa jimbo Ahmadu Fintiri alisema katika hotuba ya umma.

Uelewa wa tamaduni

‘’Serikali haiwezi kuaa kimya na kutazama vile vinavyoitwa NGs zikipotosha watu na kuchochea mielekeo ya mgawanyiko katika fikra zao,’’ aliongeza.

Tanzania pia ilikuwa na maswala na mashirika yasiyo ya kiserikali na mamlaka kufuta leseni za NGO zaidi ya 4000 kwa kile serikali ilichokiita ‘’kutofuata kanuni za fedha.’’

Nchini Uganda na Kenya, kumekuwa na madai yanayozunguka kwamba baadhi ya NGO za kigeni zinaweza kuwa zinasukuma ajenda ya mapenzi ya jinsia moja ( LGBTQ) chini ya kivuli cha programu za usaidizi wa afya.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amekuwa akitetea sheria za nchi yake dhidi ya LGBTQ. Picha: Reuters

Serikali nyingi na jamii nyingi barani Afrika zimekuwa zikipinga ajenda yoyote inayounga mkono LGBTQ ikisema ni kinyume na kanuni na maadili ya kitamaduni, kimila na kidini.

''Tumeona raia binafsi nchini Kenya pamoja na jamii nyinginezo zikikosoa usajili wa baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali nchini kwa kuzingatia dhana kwamba usajili huo ni kinyume cha maadili ya nchi na ni dhihirisho la ushawishi kutoka nje,'' asema. Wakili Muigai.

Ushawishi mbaya

Licha ya onyo la hivi punde la serikali ya Kenya kwa mashirika yasiyo ya kiserikali ''yasiyofuata sheria'', Steven Cheboi anaamini uhusiano kati ya mamlaka na mashirika yasiyo ya kiserikali kwa ujumla ni mzuri.

Baadhi ya NGO zinafanya kazi katika sekta ya afya barani Afrika kukabiliana na magonjwa. Picha: Reuters

‘’Kenya ni mfano mzuri wa jinsi NGO zinavyofanya kazi vyema na serikali. Kunaweza kuwa na nazi moja au mbili mbovu, lakini nyingi ni nzuri,’’ anasema.

‘’Tunajua kuna mambo ambayo hayaendani na utamaduni wa Kiafrika. Ni muhimu kwamba NGO ziainishe kazi na miradi yao na kanuni za kitamaduni na kijamii katika nchi,’’ anaiambia TRT Afrika.

Wakili Muigai anasema ingawa anapinga sera za kuwekea vikwazo mashirika ya NGO, anaamini kuwa mashirika hayo lazima pia yaheshimu sheria.

‘’Pamoja na kwamba mashirika yasiyo ya kiserikali yanapaswa kuruhusiwa kufanya kazi bila ushawishi, kazi zao lazima zipitie hakiki na mizani ambayo vyombo vingine pia hupitia ili kuhakikisha kuwa NGO zinabakia kweli kwa malengo yao,’’ anasema.

TRT Afrika