Anderson Duarte ni jina ambalo wachezaji wa Gambia hawatalisahau, wanapoondoka Mchuano wa kombe la dunia U-20 nchini Argentina.
Goli lake kutoka umbali wa zaidi ya mita 22, ambalo ndilo bao la pekee katika mechi hiyo, ilitosha kuwafungia nje Young Scorpions hao na kuwakatia tikiti Uruguay ya kuingia robo fainali.
Mechi hiyo ya tarehe mosi Juni kati ya Gambia na Uruguay ilitazamiwa na wengi kuwa mechi ya kuandika historia.
Iwapo Gambia wangeshinda, ingekuwa mara ya kwanza kwa nchi hiyo kufuzu robo fainali ya mchuano huu.
Uruguay sio watoto wadogo hata hivyo kwa kombe la dunia U-20, kwani wamefikia robo fainali mara 10 kati ya mara 16 walizoshiriki katika kombe hili.
Akiongea na TRT Afrika, Kocha wa Gambia, Abdoulie Bojang, "Nadhani tulionesha utendaji mzuri tena.
Kadi nyekundu ilikuja mapema katika mchezo na ilibadilisha kabisa mbinu za mchezo kwa kuwa wachezaji wetu walilazimika kukimbiza zaidi wakiwa na wachezaji wachahe. Lakini vijana walionyesha uvumilivu na ninajivunia kuwa nao."
Kazi kwa Nigeria sasa
Shambulio bila huruma kutoka kwa Nigeria iliwaacha wenyeji Argentina na butwaa walipowabandua katika mechi yao ya mchujo Jumatano, katika uwanja wa San Juan del Bicentenario.
Argentina walifungwa 2-0 kwa mabao ya Ibrahim Beji Muhammad na Rilwanu Haliru Sarki katika dakika za 61 na 92.
Katika mahojiano baada ya mechi, Ibrahim Beji Muhammad alisema kuwa timu yake ilikuwa na uhakika wa ushindi huo kabla ya kuanza mechi.
''Hili ndilo bao langu la kwanza katika mchuano huu, na nimefurahi sana. Tulikuwa tumejipanga vizuri toka mwanzo na hatukutishiwa na Argentina licha ya kuwa ndio wenyeji."
Hii ndio mara ya kwanza Flying Eagles wamefuzu robo fainali katika miaka 12 iliyopita.
Nigeria sasa wamewekeana miadi na Korea Kusini Juni 4, kutafuta nafasi ya kupenya nusu fainali.