Sudan cholera

Kwa mwaka wa pili mfululizo Sudan iko katika mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu ambao umesababisha vifo vya takriban watu 28 katika mwezi uliopita huku mvua ikinyesha katika maeneo yenye watu wengi wanaokimbia vita vilivyodumu kwa miezi 16 nchini humo, maafisa walisema.

Tangu Julai 22, wakati wimbi la sasa lilipoanza, kesi 658 za kipindupindu zimerekodiwa katika majimbo matano, mkurugenzi wa nchi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Shible Sahbani aliambia Reuters huko Port Sudan.

Pamoja na miundombinu mingi ya afya nchini kuporomoka au kuharibiwa na wafanyikazi kupungua kwa sababu ya kuhama, 4.3% ya kesi zimesababisha vifo, kiwango cha juu ikilinganishwa na milipuko mingine, Sahbani alisema.

''Zaidi ya 200,000 wako katika hatari kubwa ya kuambukizwa,'' alisema.

Vita kati ya jeshi na kikosi cha kijeshi cha Rapid Support Forces (RSF) vimezua moja ya machafuko makubwa zaidi ya kibinadamu na kusababisha zaidi ya watu milioni 10 kuwa wakimbizi ndani ya Sudan na nje ya mipaka yake.

Nchi hiyo inakabiliana na jumla ya milipuko mitano ya magonjwa ambayo ni pamoja na homa ya dengue na surua.

RSF imeendelea kuteka maeneo mengi ya Sudan, ambapo watu wamekatishwa misaada kutokana na jeshi kuwazuia na wanajeshi wa RSF kupora vifaa na hospitali.

Juhudi za kupeleka msaada katika eneo la magharibi mwa Darfur zimekuwa ngumu kutokana na mvua.

Reuters