Rais wa Uganda Yoweri Museveni amewataka waumini wa vituo vya ibada nchini humo kuwa macho hasa kutokana na tishio la shambulio la kigaidi.
Museveni aliwataka Waganda kuripoti kwa polisi watu ambao wanaonekana "sio wa kawaida" wakati wa vipindi vya ibada.
"Usiruhusu mtu yeyote usiyemjua kuingia kanisani au msikitini kwako bila kumhoji," Museveni alisema wakati wa hotuba yake kwa taifa kuhusu usalama siku ya Alhamisi.
"Usimhoji tu , bali pia wasiliana na polisi (na uwaambie) 'kuna mtu hapa ambaye hatumjui katika eneo hili'," aliongeza.
Hoteli, baa pia zimehusishwa
"Kwa hoteli na nyumba za kulala wageni, chukua maelezo ya watu wanaokuja hapo. Hakikisha wanakuonyesha vitambulisho vyao vilivyo na picha zao,” rais alisema katika hotuba yake katika Ikulu ya Nakasero.
Pia aliwataka wamiliki wa baa kuwa waangalifu, akisema: “Hakuna mtu anayepaswa kuingia kwenye baa yako. Ninyi wanywaji mnajuana.”
Matamshi yake yanakuja siku chache baada ya polisi wa Uganda kutibua shambulio la bomu kwenye kanisa kuu katika mji mkuu Kampala na baadaye kuwazuia watu kadhaa wanaodaiwa kujaribu kulipua kilipuzi katika umati wa waumini.
Mamia ya waumini walihamishwa kutoka kanisa kuu la Rubaga Miracle Centre siku ya Jumapili baada ya mshukiwa kuingia uwanjani akiwa amebeba kilipuzi, msemaji wa polisi Patrick Onyango alisema.
Uchunguzi wa tukio hilo unaendelea, polisi walisema.