Mwenyekiti wa Baraza la mpito Sudan, Luteni Jenerali Abdel Fattah Al-Burhan ameondoka mapema leo kuelekea jiji la New York, Marekani, akiongoza ujumbe wa taifa la Sudan utakaoshiriki rasmi kwenye kikao cha sabini na nane cha mkutano mkuu wa Baraza la Umoja wa mataifa, UN.
Al-Burhan anatarajiwa kutoa hotuba yake kuhusu hali ya Sudan mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA.
Kiongozi huyo alisindikizwa kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Port Sudan Na viongozi mbalimbali wa nchi hiyo wakiongozwa na Makamu wa Rais wa Baraza la Mpito Malik Aqar Air, na Luteni Jenerali Muhammad Al-Ghali Ali Youssef.
Siku ya Ijumaa wiki hii, kiongozi huyo anatarajiwa kushiriki katika mikutano ya ngazi ya juu kujadili kuimarisha ushirikiano wa kimataifa kuhusiana na masuala mbalimbali ya kimataifa na kikanda.
Aidha, Luteni Jenerali Abdel Fattah Al-Burhan atafanya mazungumzo na marais kadhaa na wawakilishi mbalimbali kutoka nchi tofauti za ulimwengu yakiwemo mashirika ya kimataifa na kikanda kandokando ya kikao hicho cha 78 cha Umoja wa Mataifa.
Katika siku za hivi karibuni, Al-Burhan amefanya ziara katika nchi mbalimbali ikiwemo Qatar, Sudan Kusini, Uganda, Uturuki na Misri zikiwa na lengo la kutafuta ushawishi wa kuungwa mkono dhidi ya kikundi cha RSF ambacho amekuwa katika mapigano nacho tangu tarehe 15 mwezi Aprili mwaka huu.