Kiongozi wa kijeshi wa Niger Jenerali Abdourahmane Tiani anasema nchi hiyo itaendeleza mchakato wa mpito ambao hautadumu kwa muda usiozidi miaka mitatu na kuonya kuwa shambulio lolote dhidi ya nchi hiyo halitakuwa rahisi kwa waliohusika.
"Matarajio yetu sio kunyang'anya mamlaka," Jenerali Abdourahamane Tchiani alisema katika hotuba yake kwenye televisheni. Muda wa mpito wa madaraka "hautazidi zaidi ya miaka mitatu", alisema.
Kiongozi huyo wa serikali pia alitangaza kipindi cha siku 30 cha "mazungumzo ya kitaifa" kuandaa "mapendekezo madhubuti" ili kuweka misingi ya "maisha ya katiba mpya".
Jenerali Tchiani ambaye alikuwa mkuu wa Walinzi wa Rais wa Niger, alimwondoa bosi wake Mohamed Bazoum mnamo Julai 26 na kuzua shutuma za kimataifa na shinikizo la kumtaka aachie madaraka.
Hotuba yake ilifuatia mkutano na wajumbe kutoka kambi kuu ya kanda ya Afrika Magharibi ECOWAS.
Tayari kwa mashauriano
Timu ya ECOWAS pia ilikuwa imekutana na rais aliyepinduliwa Bazoum wakati wa ziara yake katika mji mkuu Niamey siku ya Jumamosi. Ujumbe huo ulisafiri hadi Niamey kutafuta suluhu la amani badala ya kijeshi baada ya maafisa wakuu wa jeshi kunyakua mamlaka katika mapinduzi.
Ziara ya timu hiyo inayoongozwa na rais wa zamani wa Nigeria Abdulsalami Abubakar inajiri siku moja baada ya wakuu wa jeshi la ECOWAS kutangaza kuwa wako tayari kuingilia kati kumrejesha madarakani rais aliyeondolewa madarakani.
Kiongozi wa junta alisema wako tayari kwa mazungumzo na hawataki vita lakini kwamba watailinda nchi yao ikiwa kuna uingiliaji wowote wa kijeshi.
"Ikiwa shambulio lingefanywa dhidi yetu, haitakuwa rahisi kama baadhi ya watu wanaonekana kufikiria," Tchiani alisema.
Mkuu wa ujumbe wa ECOWAS, Abdulsalami Abubakar aliwaambia waandishi wa habari kwamba ''hatua imefanywa'' na ''mazungumzo yataendelea.'' Alisema Rais aliyeondolewa madarakani Bazoum aliwafahamisha kuhusu ''baadhi ya matatizo'' aliyokuwa akikabiliana nayo kutokana na mabaya aliyotendewa.''
Mpatanishi wa ECOWAS hakutoa maelezo lakini alisema watatoa mrejesho kwa Rais wa Nigeria Bola Tinubu ambaye ni mwenyekiti wa jumuiya hiyo ya kikanda.
Hatua ya mwisho
Hii ni mara ya kwanza kwa timu ya ECOWAS kukutana na kiongozi wa junta na rais aliyeondolewa madarakani. Majaribio yao ya hapo awali yalikataliwa na watawala wa kijeshi.
Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) imekubali kuweka tayari "kikosi cha kusubiri" kama suluhu la mwisho la kurejesha demokrasia nchini Niger baada ya majenerali kumweka kizuizini Rais Mohamed Bazoum Julai 26. Lakini inasema inapendelea mazungumzo ili kutatua mgogoro huo.
Kumekuwa na wito wa kimataifa kuwataka watawala wa kijeshi kuachia madaraka lakini wameshikilia msimamo mkali hadi sasa.
Jumuiya ya kikanda ya ECOWAS imeweka vikwazo vya kiuchumi dhidi ya nchi hiyo kama sehemu ya shinikizo hilo huku mamlaka ya kijeshi ikielezea vikwazo kama vile ''haramu'' na ''isiyo ya haki'' ikitaja athari zake kwa raia.