Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken amejadili umuhimu wa kumaliza vita nchini Sudan na mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan, wizara ya mambo ya nje ya Marekani ilisema siku ya Jumanne.
Wawili hao walijadili hitaji la kumaliza machafuko hayo nchini Sudan ili kuruhusu misaada ya kibinadamu kutolewa kwa wakati," alisema Matthew Miller, msemaji wa wizara hiyo katika taarifa.
Katika mazungumzo hayo yaliyodumu kwa dakika 30, Blinken aligusia kufufuliwa kwa kwa usuluhishi wa Jeddah na umuhimu wa kuwalinda raia na kupunguza machafuko huko El-Fasher, kaskazini mwa Darfur," alisema Miller.
Katikati ya mwezi Aprili, Marekani ilisema kuwa mazungumzo ya amani yataandaliwa na Saudi Arabia katika mji wake wake wa Jeddah ndani ya wiki tatu zijazo, ingawa tarehe kamili haikuwekwa wazi.
'Ukurasa wa kutisha'
Takribani watu 134 wameuwawa ndani ya wiki mbili za mapigano yaliyoukumba mji wa El-Fasher, kulingana na takwimu zilizotolewa siku ya Jumapili na Madaktari Wasio na Mipaka(MSF).
Tangu Aprili 2023, Sudan imekuwa ikikabiliwa na vita kati ya jeshi, linaloongozwa na Burhan, na makamu wake wa zamani, Mohamed Hamdan Dagalo, anayeongoza kikosi cha RSF.
El-Fasher huko Darfur Kaskazini ni mji pekee ambao hauko chini ya udhibiti wa RSF, na ni kitovu muhimu cha kibinadamu kwa kanda iliyo kwenye baa la njaa.
Kulingana na Umoja wa Mataifa, machafuko hayo tayari yameua maelfu ya watu.