Kesi ya watu 25 wanaotuhumiwa kuwa sehemu ya kundi la M23 ilianza Jumatano huko DR Congo, takriban miaka miwili na nusu baada ya waasi kuanza kushika sehemu kubwa za mashariki mwa nchi.
Ni watuhumiwa watano tu waliohudhuria wakati kesi ilipoanza katika mahakama ya kijeshi katika mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Kinshasa.
Mshtakiwa mkuu, rais wa zamani wa tume ya uchaguzi ya DRC Corneille Nangaa, kwa sasa yuko mafichoni.
Nangaa alitangaza Desemba huko Nairobi kuundwa kwa harakati za kisiasa-kijeshi zinazojulikana kama AFC, au Alliance Fleuve Congo, muungano wa makundi ya waasi ikiwa ni pamoja na M23.
Adhabu ya kifo
Wizara ya haki ilitangaza Jumatatu kufunguliwa kwa "kesi ya Corneille Nangaa na washirika wake."
"Kesi hii ni sehemu ya shughuli za kigaidi, uhalifu wa kivita na uhaini mkubwa uliotekelezwa katika sehemu ya mashariki ya DRC," taarifa ilisema.
Ikiwa watapatikana na hatia, wanaweza kukabiliwa na adhabu ya kifo.
Upande wa utetezi uliomba kesi iahirishwe baada ya mtuhumiwa wa kwanza kuhojiwa ili kuruhusu mawakili muda wa kusoma mafaili ya wateja wao.
'Haki ya usawa'
"Muda tuliotengewa ni mfupi sana, katika kesi nzito kama hii, ambayo baadhi ya watuhumiwa wanaweza kukabiliwa na adhabu ya kifo," mmoja wa mawakili wa utetezi, Clement Muza Kayembe, alisema.
Mwanasheria huyo pia alizungumzia uwepo wa Waziri wa Haki Constant Mutamba katika kesi hiyo.
"Ni nchi gani umewahi kuona waziri wa haki akienda kwenye vikao vya kusikiliza kesi?" aliambia AFP.
"Ni shinikizo la kimaadili," alisema, akiomba "haki ya usawa na si haki ya kufikirika" kwa watuhumiwa.
Kuhukumiwa huku ukiwa haupo
Orodha ya watuhumiwa inajumuisha baadhi ya watu mashuhuri wa M23, wakiwemo rais wa kundi hilo Bertrand Bisimwa, kiongozi wake wa kijeshi Sultani Makenga na wasemaji Willy Ngoma na Lawrence Kanyuka.
Watu wengine waliotajwa kwenye orodha hiyo ni pamoja na wanachama wa Chama cha Watu kwa ajili ya Ujenzi na Demokrasia (PPRD) ambao walijiunga na AFC.
PPRD ni chama cha Rais wa zamani Joseph Kabila, ambaye alikuwa madarakani kutoka 2001 hadi 2019.
Wale ambao hawajahudhuria kesi watahukumiwa kwa kutokuwepo.
Tukio la mabomu
Mamlaka za Congo zinamtuhumu Nangaa kuwa nyuma ya ulipuaji wa kambi ya wakimbizi wa ndani mwezi Mei uliopita ambao uliua watu 35.
Kesi hiyo inatarajiwa kuendelea Alhamisi.
M23 ("Vuguvugu la Machi 23") walianza vurugu tena mwishoni mwa mwaka 2021 na kushika maeneo makubwa ya jimbo la Kivu Kaskazini.