Kenya imewatuma kundi la kwanza la walimu 67 nchini Marekani katika mpango wa ajira ya kitaaluma katika nafasi mbali mbali za shule nchini humo.
Akiwahutubia walimu walioandamana na familia na marafiki, Waziri wa mambi ya nje Musalia Mudavadi alisema serikali inajivunia kuona kundi la kwanza la walimu likipata ajira Marekani.
"Leo, tunatuma kwa fahari kundi la walimu wa Kenya ambao wamepata nafasi za kazi katika shule mbalimbali za wilaya kote Marekani," alisema Mudavadi.
Mudavadi aliwasifia walimu hao kama mabalozi wa Kenya watakaoinua hadhi ya taifa na viwango vya elimu vya Kenya katika ngazi ya kimataifa.
"Lazima tukumbuke kila wakati kuwa wakati unapokuwa kwenye ndege hiyo na unatua, uko katika mamlaka tofauti, na lazima ufuate sheria na kanuni ili usitue kwa upande mbaya wa sheria," Mudavadi. sema.
Serikali imesisitiza kuwa itaendelea kulinda haki na ustawi wa wanadiaspora wa Kenya na kuunganisha michango yao muhimu katika michakato ya ujenzi wa nchi.
Haya yanajiri baada ya ripoti kuwa maelfu ya walimu walijiuzulu kutoka kwa Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) na kutia saini kandarasi za kwenda Uingereza na Marekani.
Uingereza na Marekani wanadaiw akutangaza zaidi ya nafasi 400,000 za kazi za walimu katika awamu mbali mbali huku zikipendekeza marupurupu bora zaidi yanayovutia ikiliinganishwa na yanayotolewa na serikali ya Kenya.
Wakizungumza na waandishi wa habari, baadhi ya walimu hao walitaja kucheleweshwa kwa upandishaji vyeo kutoka TSC, ukosefu wa miundombinu, na hitaji la elimu zaidi ili kupandishwa madaraja kuwa sababu zinazosababisha kuhama kwa wingi.
Kenya imekuwa ikituma wafanyakazi wa taaluma mbali mbali katika nchi za ngambo, ikiwemo Uingereza, Ujerumani, Marekani, Saudi Arabia nyengine.
Mapema wiki hii, Rais William Ruto, ambaye yuko katika ziara ya pwani ya nchi, aliahidi kuwa serikali yake itawasaidia Wakenya wanaotafuta ajira ng'ambo, ikiwemo kuwalipia nauli za ndege na usaidizi mwengine kama kupata visa za kusafiria.
Hii inakuja wakati Rais huyo anajaribu kutuliza jojto la hasira miongoni mwa vijana maarufu kama Gen Z waliokuwa wakiandamana na kuvuruga shughuli za serikali wakilalamikia ugumu wa maisha na tozo za juu pamoja na ukosefu wa ajira kwa vijana.
''Nimefanya kila niwezalo, nimewatafutia aira ng'ambo na nimehakikisha mtapata hati za usafiri ndani ya wiki moja,'' alisema Rais Ruto. ''Sasa bidii kwenu,'' Ruto aliwaambia umati aliohutubia.
Walimu wa Kenya wamekuwa wakilumbana na serikali kutokana na mishahara duni pamoja na upungufu mkubwa wa walimu katika shule za nchini na ukosefu wa vitendea kazi ikiwemo madarasa ya kutosha.
Kwa mujibu wa tume wa kuwaajiri walimu nchini TSC, Kenya ina uhaba wa zaidi ya walimu 50 000 hasa katika shule za sekondari.