Rais wa Kenya William Ruto amewapa uraia watu wa jamii ya Wapemba wasio na utaifa, ambao walitambuliwa rasmi tu kati ya makabila ya nchi hiyo mnamo Februari.
Uraia utawapa kundi hilo “kitambulisho na utambuzi wanaostahili” na kuruhusu jamii kupata huduma za umma, Rais Ruto alisema.
"Hii, kwa hakika, inamaliza hali ya watu wa Pemba kutokuwa na utaifa na kutengwa ambao umedumu kwa takriban miaka 100," alisema wakati wa hafla ya Ijumaa.
Jamii ya Wapemba inakadiriwa kuwa takriban 7,000 kwa idadi na wamejikita katika maeneo ya pwani ya Kenya ya Kwale, Kilifi, Mombasa na Lamu.
Rais alitoa vitambulisho, vyetu vya umiliki wa ardhi, vyeti vya kuzaliwa na hati za kusafiria katika hafla iliyoashiria kukamilika kwa mchakato wa usajili wa wanajamii wote.
Hatua hiyo hatimaye inawawezesha Wapemba kupata huduma kamili za umma kama shule, huduma za afya, hifadhi ya jamii na haki ya kufanya kazi ambayo wamekuwa wakinyimwa kwa muda mrefu.
Jamii hiyo iliishi Kenya takriban karne moja iliyopita lakini haikutambuliwa kamwe wakati wa uhuru mnamo 1963.
Inaaminika awali walitoka kisiwa cha Pemba katika Visiwa vya Zanzibar vilivyoko Tanzania Bara.