Rais wa Kenya William Ruto ametoa ajenda yake kuu ya uongozi wa Jumuiya ya Kanda ya Afrika Mashariki EAC, akitaja usalama, uwajibikaji wa kisiasa, na uwekezaji kama vigezo muhimu katika ufikiaji wa Afrika Mashariki thabiti.
Rais Ruto aliyasema hayo alipopokea uenyekiti wa Jumuiya hiyo kutoka kwa Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini aliyeshikilia kwa muda wa mwaka mmoja.
''Ninaahidi kufanya kazi kwa bidii pamoja na kila mmoja wenu ili kuendeleza maono na dhamira yetu Jumuiya,'' alisema Rais Ruto.
'Utofauti wetu ni nguvu yetu'
Rais Ruto pia aliwataka wanachama kukumbatia utofauti wa mataifa kama njia ya kuwaleta pamoja.
''Ushirikiano wa uchumi wetu, kuoanisha sera zetu, na kusherehekea utofauti wetu yatafungua sana fursa kwa ustawi wetu wa pamoja,'' aliongeza.
Miongoni mwa ahadi zake kwa Jumuiya, Rais Ruto alisema ataweka kipaumbele kuboresha ubora wa maisha kwa watu wa Afrika Mashariki, kwa kutilia mkazo ushindani, kukuza uzalishaji wa ongezeko la thamani, kukuza biashara ya ndani ya kikanda, na kuendesha uwekezaji.
'' Hizi ni nguzo muhimu kwa kubadilisha uchumi wetu, kutengeneza nafasi za kazi, na kuhakikisha maendeleo endelevu katika kanda nzima,'' hotuba ya Rais Ruto ilisema.
Ukuaji kibiashara
Afrika Mashariki imetakiwa kukuza mazingira yatakayochochea utanuzi wa biashara sio ndani tu bali hata nje ya kanda na nje ya bara kwa jumla.
Katika hotuba yake ya kwanza kama Mwenyekiti wa EAC, Rais William Ruto aliwahimiza viongozi waliokuwepo kujitahidi kuondoa vikwazo vya ndani ya nchi kwa wafanyabiashara na kulenga kuunda uhusiano wa usawa kibiashara na mataifa tajiri.
''Natoa wito kwa Sekretarieti ya EAC kuongeza nguvu katika majadiliano na Umoja wa Ulaya ili kuwezesha ushirikishwaji wa Nchi zote Wanachama katika mfumo wa biashara uliounganishwa.''
Kwa mtazamo wake, Rais Ruto anasema hii ita itaimarisha uwezo wa kujadiliana, kupanua ufikiaji wa masoko, na kuiweka EAC kama kambi ya kiuchumi ya kuheshimika.
Ruto atashikilia wadhifa wa Mwenyekiti wa Jumuiya hadi wakati kama huu mwakani.
Ushauri wa Kiir akiachia Uenyekiti
Rais anayeondoka wa Jumuiya, ambaye ni Rais wa Sudan Kusini, aliwashauri wanachama kuendelea juhudi za upatanishi katika kand ili kuondoa mizozo na migogoro inayovuruga maendeleo.
''Nimejionea na kuathirika moja kwa moja na vita. Nimeona athari za uharibifu za vita kwa raia na kwa nchi,'' alisema Rais Kiir.
Ni kwa muktadha huu, ndio anasema uenyekiti wake ulijikita katika midahalo muhimu kuhusu amani na usalama katika eneo.
Katika ushauri wake, Rais Salva Kiir pia alisisiti zaumuhimu wa kuwekeza katika ukuzaji na upanuzi wa biashara ndani ya Jumuiya, kusukuma ajenda ya sarafu moja kwa wananchama na kujenga uwezo wa kustahimili hali ya hewa na kuwawezesha vijana kupitia ubunifu na biashara huria.