Mashindano haya yanajumuisha mataifa 53.Kenya imetuma kikosi cha wanariadha 73, Picha Tim Olobulu (for TRT Afrika)

Kenya imejitosa kichwa kichwa katika mashindano ya ufukwe yanayofanyika mjini Hammamet Tunisia kwa ushindi dhidi ya Algeria katika mpira wa mikono upande wa wanawake.

Magwiji Michelle Adhiambo na Brenda Ariviza waliongoza timu ya Kenya kwa jumla ya alama nane na sita mtawalia kuipatia Kenya ushindi wa 2-1 dhidi ya Algeria.

Algeria walianza kwa mikiki na kuwapa wakenya uongozi wa kejeli kwa kuwapiga alama nane kwa sufuri dakika za mwanzo tu za mechi lakini kenya wakajiuliza na kujijibu na matokeo kujitokeza.

‘’Katika dakika tatu au nne za kwanza tuligundua makosa yetu yalikuwa wapi. Tukaomba mapumziko mafupi na tukabadilisha mkakati wetu;’’ anasema nahodha wa timu ya Kenya Michelle Adhiambo.

Kenya itachuana na na Mali na Uganda Jumapili kutafuta kuingia fainali  Picha Tim Olobulu (for TRT Afrika)

Timu tano za wanawake zinachuana katika mzunguko wa mechi ambapo kilele itakuwa fainali ya medali kati ya timu mbili bora zaidi.

Mashindano hayo yaliyoanza Jumamosi 24 yataendelea hadi Juni 30, na kuleta pamoja zaidi ya wanamichezo 1000 kutoka mataifa takriban 50.

Michezo 15 tofauti zitashindaniwa ikiwemo riadha, mpira wa vikapu, shindano la maboti, voliboli, na uogeleaji, miongoni mwa nyingine.

Ushindi huu katika shindano la kwanza la Kenya, unawapatia kikosi cha taifa hilo la Afrika Mashariki motisha katika mechi wanazokabiliana nazo.

‘’Inatia motisha sana, kujua kuwa sasa tuna kitu cha kukihifadhi, nacho ni nafasi yetu ya uongozi kwa sasa,’’ anasema Skipa wa Kenya Adhiambo. ‘’Tupo juu katika jedwali, Kwa hiyo lazima tuilinde nafasi hiyo kwa vyovyote vile.’’

Adhiambo na kikosi chake watakutana na Mali siku ya Jumapili katika mechi yao ya pili kisha kupambana na majirani zao Uganda Jumapili jioni katika mechi yao ya tatu.

Kenya imetuma kikosi cha watu 73 huku Ghana ikituma wanne, ikiwa ndilo taifa lenye wachezaji wachache zaidi na wenye umri mdogo zaidi.

Haya ni mashindano ya pili ya ufukwe ya Afrika kuandaliwa, miaka minne baada ya Cape Verde kuandaa ya kwanza 2019.

TRT Afrika