Usitishaji vita wa masaa 72 uliotarajiwa nchini Sudan kuanzia Ijumaa, umeripotiwa kufeli, huku kukiwa na ripoti kwamba majeshi ya angani yanaendelea kupambana mashariki mwa Khartoum.
Huku ikiendelea kuitisha amani kwa jirani yake Sudan , Kenya imejitolea kuwa mwenyeji wa mazungumzo ya amani kati ya jeshi la Sudan na Vikosi vya Rapid Support Forces, RSF.
"Kenya inajitolea kuandaa mchakato wa upatanishi kati ya wahusika katika makubaliano," taarifa ya Ikulu ya Kenya inasema, "tunajitolea hivi kwa nia ya undugu, amani na mshikamano kama mchakato unaokubalika wa kutoegemea upande wowote na pia kama mshikadau ambaye anafuatilia mzozo katika nchi ya Sudan”
Kenya, Sudan Kusini na Djibouti zilichaguliwa na mamlaka ya Kiserikali ya Maendeleo, IGAD, kuwa wapatanishi katika mzozo wa Sudan.
Mfanyakazi wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, IOM, aliripotiwa kuuawa siku ya Ijumaa wakati gari alilokuwa akisafiria pamoja na familia yake ilikutana na mzozo kati ya vikosi vya kijeshi vinavyopambana.
"Mlipuko wa hivi punde wa ghasia umeilazimu IOM kusimamisha shughuli zake za kibinadamu nchini Sudan. Pande zote lazima zihakikishe misaada ya kibinadamu zinaweza kupitishwa ili kusaidia wale walio hatarini zaidi," IOM imesema katika taarifa yake.
Siku ya Ijumaa, RSF, walisema wako tayari kufungua viwanja vyote vya ndege nchini Sudan kwa upendeleo ili kuruhusu usafiri wa anga kwa nchi ambazo raia wake wanataka kuondoka.