Polisi nchini Kenya wamerejelea shughuli ya kufukua maiti katika msitu wa Shakahola, uliopo mji wa Malindi, pwani ya Kenya.
Waziri wa Usalama wa ndani Kithure Kindiki, ameelezea wanahabari kuwa, kufikia Jumanne mchana, vyombo vya usalama vimeweza kuwaokoa watu 65 waliokua bado katika msitu huo wakiwemo watoto, japo hakuelezea idadi kamili ya watoto.
‘‘Ninahofia kuwa huenda kukawa na maiti zaidi katika msitu huu. Hii imefanya tuamini kuwa, mauaji haya yalikuwa yamepangwa.’’
Bw. Kindiki pia amesema kuwa polisi wameendelea kauwahoji mamia ya washukiwa wanaosaidia katika upelelezi juu ya ‘maiti zilizokutwa’ katika msitu huo tangu mwezi Aprili, na kuwaacha wengi na mshtuko.
Wakati huo huo, kiongozi wa upinzani Raila Odinga amewasilisha kesi mahakamani dhidi ya rais William Ruto, akimshutumu kwa kuvuka mipaka yake na kuingilia kazi isiyomhusu ya upelelezi wa uhalifu.
Raila amesema rais Ruto hana mamlaka yoyote kuteua jopo hilo la kufanyia uchunguzi mauaji ya Shakahola, wakati kuna idara ya polisi, na mashirika mengine ya haki yanayohusika.
Katika shtaka lake hilo, Raila ameiomba mahakama kubatilisha uteuzi wa jopo hilo mara moja. Viongozi wa muungano wa makanisa pia walipinga uteuzi huo wa wanachama 17 waliotarajiwa kuanza vikao vyao wiki hii.
Kwingineko polisi wamesema kuwa wametambua sehemu zingine takriban 20 ndani ya msitu huo ambako kunashukiwa huenda kukapatikana maiti zaidi.
Kufikia Jumanne, maiti 112 zilikuwa zimefanyiwa uchunguzi na mwana patholojia wa serikali lakini kufuatia shughuli iliyorejelewa ya kufukua makaburi, inahofiwa idadi hiyo ikaongezeka mara dufu.
Oparesheni ya polisi kufukua makaburi ilisitishwa awali kutokana na mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha.