Kinara wa Azimio Raila Odinga amesitisha maandamano tayari kwa mazungumzo na mrengo unaotawala wa Rais Ruto / Picha: AFP

Mrengo wa Azimio nchini Kenya ukiongozwa na Raila Odinga umetoa taarifa hii leo kusema wako tayari kwa mazungumzo ya amani kama ilivyopendekezwa ili kusuluhisha baadhi ya changamoto zilizosababisha maandamano yaliyoshuhudiwa nchini humo.

Awali, upande wa serikali kupitia msemaji wao Kimani Ichungwah, ulishikilia kuwa mazungumzo hayo hayatohusisha uundwaji wa serikali ya mseto maarufu 'nusu mkate'.

Kimani ambaye pia ni kiongozi wa walio wengi bungeni, ameyataka mazungumzo hayo yapeperushwe moja kwa moja ili kuwawezesha Wakenya kushiriki na kufahamu hoja za upinzani kwani mazungumzo hayo yanahusu maisha ya Wakenya.

Muungano huo umemteua aliyekuwa naibu rais nchini Kenya Kalonzo Musyoka kuongoza mazungumzo ya upande wake huku akisaidiwa na mbunge Opiyo Wandayi ambaye pia ameteuliwa kama msemaji wao.

Ahadi yetu ya kujadiliana kwa nia njema, yenye lengo la kutatua changamoto za taifa kwa kina kupitia mazungumzo, bado haijayumba. Tunatetea mazungumzo ya uwazi, yenye heshima, yanayofaa yakiongozwa na uadilifu, na heshima kwa watu wa Kenya.

Azimio

Muungano wa Azimio umeongeza kuwa ulisitisha maandamano yake ili kutoa fursa ya mazungumzo ya amani kwani unaamini kuwa taifa la Kenya linastahili maelewano, na hivyo basi kuwaalika raia wa nchi hiyo na jumuiya ya kimataifa kuwawajibisha.

Ajenda za kujadiliwa

Kati ya mwezi Juni na Julai, Kenya ilishuhudia ghasia kufuatia maandamano ya muungano wa upinzani uliopinga kupitishwa bungeni kwa mswada wa sheria ya fedha inayodaiwa kuzidisha gharama ya maisha kufuatia ushuru wa juu kwa bidhaa muhimu.

Aidha, Muungnao wa Azimio umetaja ajenda za mazungumzo yake kuwa: 'Gharama ya maisha, Ukaguzi wa matokeo ya uchaguzi wa Rais wa 2022, Marekebisho na uundaji upya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka na Mambo yanayohusiana Nayo, Hatua za kuzuia kuingilia vyama vya kisiasa, Masuala ya Kikatiba ambayo Hayajakamilika.

Upande wa serikali haujatoa ajenda upande wao isipokuwa kusisitiza kwamba liwalo n aliwe hawako radhi kugawana mamlaka na upinzani.

Kikosi kazi

Kulingana na Azimio, wawakilishi wake kwenye mazungumzo hayo watasalia jinsi ilivyowatangaza awali.

  • Stephen Kalonzo Musyoka – Kiongozi wa Ujumbe
  • James Opiyo Wandayi – Kiongozi wa walio chache bungeni
  • Eugene Wamalwa – Kiongozi wa chama cha DAP
  • Okongo Omogeni - Seneta
  • Amina Mnyazi - Mbunge

  • Wawakilishi wa Kenya Kwanza kwenye mazungumzo ni;
  • Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung'wah
  • Seneta Aaron Cheruiyot.
  • Gavana wa Embu Cecily Mbarire
  • Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) Hassan Omar
  • Mwakilishi wa Wanawake wa Bungoma Catherine Wambilianga.

Wakati huo huo, upinzani umepinga vikali shutuma dhidi yake kutoka kwa Inspekta Jenerali Mkuu wa polisi nchini humo Japheth Koome ambaye amewalaumu kwa kutumia miili ya maiti kutoka vyumba vya kuhifadhia maiti na kudai ni waathiriwa wa utumiaji wa nguvu kutoka polisi kwenye ghasia za hivi majuzi.

TRT Afrika