Paul Mackenzie alijiita kiongozi wa kidini akafungua Kanisa la Good News International mwaka wa 2003, lakini miaka kumi baadaye miili inafukuliwa katika msitu wa Shakahola, pwani mwa Kenya, ambapo anaripotiwa aliwashawishi watu kuhamia na kujinyima chakula kwa ajili ya kumuona Yesu.
Tangu Mwezi Aprili mwaka huu miili 240 imefukuliwa kutoka kwa ardhi hiyo yenye ukubwa wa ekari 800.
Waziri wa mambo ya ndani na utawala wa kitaifa nchini Kenya, Kithure Kindiki, anasema awamu ya pili ya uchunguzi ya maiti zilizofukuliwa kutokana na mauaji katika msitu wa Shakahola utaanza tena tarehe 24 Jumatano katika hospitali ndogo ya Malindi nchini Kenya.
" Utafutaji wa makaburi na uchimbaji wa miili kwa sasa umesitishwa ili kuruhusu upangaji wa vifaa vya uchunguzi wa ziada wa miili 123 iliyopatikana katika awamu ya kwanza ya ufukuaji," Kindiki ameelezea.
Lakini utafutaji na uokoaji wa manusura ndani ya msitu wa Shakahola na eneo la Chalkama kwa ujumla utaendelea bila kukatizwa.
Utafutaji utafanywa hadi kwenye kingo za mbuga jirani ya Tsavo mashariki katika siku zijazo kwa kutumia maelezo ya watu na ndege zisizo na rubani.
Wakati huo huo mahakama kuu nchini Kenya imesitisha shughuli za tume ya uchunguzi iliyoteuliwa na rais William Ruto kwa siku saba.
Tume hii ilifaa kuchunguza vifo, utesaji, unyanyasaji wa kinyama na udhalilishaji wa waathiriwa wanaohusishwa na Kanisa la Good News International la Kilifi- linalohusishwa na mchungaji Paul Mackenzie.
Hii ni baada ya chama cha Upinzani , muungano wa Azimio kuwasilisha kesi hiyo wiki mbili zilizopita ukisema kuwa uteuzi wa Rais William Ruto wa timu hiyo ya wanachama wanane ni kinyume cha sheria na ni sawa na unyakuzi wa mamlaka yaliyopewa vyombo vingine vya serikali na Katiba.