Shule zilitarajiwa kufunguliwa tangu Aprili 29 lakini rais alitangaza kuahirishwa kufunguliwa kutokana na hatari iliyokuwepo./ Picha: Reuters

Hata hivyo vyombo vya usalama vimetakiwa kutoa ulinzi na usaidizi kuhakikisha usalama wa wanafunzi na walimu wakati wa kurudi shuleni.

''Serikali inaendelea kufuatilia hali ya mafuriko nchini na itahakikisha wanafunzi, wazazi na walimu wanapita kwa usalama na kwa ufanisi shule zitakapofunguliwa kwa muhula wa pili,'' amesema waziri wa usalama wa ndani Kithure Kindiki.

Waziri pia aliwataka wazazi kuwa waangalifu wanapowapeleka watoto shuleni.

''Wizara inatoa wito kwa wazazi kuhakikisha usalama wa watoto hao kwenda na kurudi shuleni kati ya saa kumi na mbili asubuhi hadi saa kumi na mbili jioni, jambo ambalo linapaswa kufanyika kwa ushirikiano wa karibu na timu za Mashirika mbalimbali na uongozi wa shule,'' aliongeza Kindiki.

Kenya imepokea mvua kubwa kupita kiasi katika miezi michache iliyopita na kusababisha mafuriko katika maeneo mengi.

Shule zilitarajiwa kufunguliwa tangu Aprili 29 lakini rais alitangaza kuahirishwa kufunguliwa kutokana na hatari iliyokuwepo.

Pia baadhi ya shule ziligeuzwa kuwa makao ya muda kwa waathiriwa wa mafuriko, ambao nyumba zao zilisombwa au zimo katika hatari ya kusombwa.

Duru zinasema kuwa uamuzi wa kufunguliwa shule ulifikiwa kufuatia ushauri kutoka kwa Idara ya Hali ya Hewa ya Kenya.

Zaidi ya watu 300 wanahofiwa kufariki katik amafuriko hayo Kenya huku takriban nusu milioni wakiachwa bila makao au kulazimika kuhamia maeneo salama.

Hata hivyo, kwa baadhi ya maeneo ambapo hali bado ni hatari sana, serikali ilisema itachelewesha kufunguliwa kwa shule hizo.

''Shule ambazo zimeathiriwa vibaya na mvua kubwa na mafuriko ambayo yamesababisha maelfu ya watu kuyahama makazi yao katika maeneo mbalimbali ya nchi yatacheleweshwa kufunguliwa ili serikali ifanyie ukarabati unaohitajika,'' alisema waziri Kindiki.

Kenya ina takriban wanafunzi milioni 15 wa shule za msingi na sekondari.

TRT Afrika