Miili ya wanafunzi 19 ilipatikana kwenye eneo la tukio, huku wengine wawili wakifariki dunia baada ya kufikishwa hospitalini, taarifa ya Polisi nchini Kenya imesema.
Kufikia Ijumaa, idadi ya waliopoteza maisha katika tukio hilo lililotokea katika shule ya msingi ya Hillside Endarasha ilikuwa ni 17, hata hivyo kulingana na taarifa kutoka serikalini, idadi hiyo sasa imefikia 21.
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini Kenya Resila Onyango alisema kuwa moto huo ulikuwa umedhibitiwa ingawa hakutoa chanzo cha ajali hiyo.
Baada ya moto huo kudhibitiwa, polisi walitumia mwanga katika kutafuta manusura wa tukio hilo.
Moto mwingine
Siku ya Jumamosi, wanafunzi wengine walijeruhiwa na mali kuharibika kufuatia tukio la moto lililotokea katika Shule ya wasichana Isiolo, Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Kenya limesema.
"Tukio la moto limeripotiwa katika shule ya sekondari ya wasichana ya Isiolo iliyoko kaunti ya Isiolo," Shirika la Msalaba Mwekundu la nchi hiyo limesema katika ukurasa wake X siku ya Jumamosi.