Hali ya joto kali inashuhudiwa kote Asia, kaskazini mwa Afrika, Ulaya na Marekani huku watu wakijaribu njia za kujituliza.
Morocco, Misri na Algeria zimerekodi baadhi ya viwango vya juu vya joto barani Afrika. Nchi zote hizi zinakabiliwa na hatari ya kupungua viwango vya maji mwilini huku kukiwa na wasiwasi wa afya ya umma.
Watu wamekuwa wakijazana katika fukwe za kusini mwa Ulaya na Amerika ambapo halijoto ya kuvunja rekodi inatarajiwa katika siku zijazo.
Mamlaka imeshauri matumizi zaidi ya maji na watu waepuke pombe na kahawa ambazo zinapunguza maji mwilini.
Nchini Italia, mamlaka imewashauri watu kuwatunza hasa wazee kwa sababu ya halijoto ya juu.
Wapalestina huko Gaza wamekuwa wakielekea kwenye ufuo wa bahari kujipoza huku wazazi wakiwamwagilia watoto maji kutoka kwa mabomba kutokana na wimbi la joto.
Joto kali linafanya maisha kuwa magumu zaidi kwa familia maskini zinazoishi katika nyumba za kupanga.
Zaidi ya watu milioni 2.3 wamejaa kwenye ukanda wa Gaza. Kitongoji cha al-Nasr kina watu wanaoishi katika nyumba duni na hawawezi kumudu vifaa vya kupoeza. Wakazi wengi hukaa nje na kutafuta maji ili kukabiliana na joto.
Mkoa wa Allahabad nchini India umekuwa wenye joto zaidi nchini humo. Wanaume wameamua kujipaka tope kwenye miili yao ili kujipoza kwenye kingo za mto Ganges.
Halijoto katika Allahabad inatarajiwa kufikia nyuzi joto 44 (digrii 111.2 Fahrenheit), kulingana na tovuti ya idara ya vipimo vya vipimo vya India.
Wataalamu wanasema joto kali linalokumba mataifa mengi duniani ni ishara tosha ya tishio la ongezeko la joto duniani.