Karibuni Uswahilini : Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aipongeza Malawi kwa kuanza kufundisha kiswahili shuleni

Karibuni Uswahilini : Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aipongeza Malawi kwa kuanza kufundisha kiswahili shuleni

Malawi inasema kuwa kiswahili kitasaidia biashara kati yake na mataifa jirani
Rais wa Tanzania Mh Samia Suluhu Hassan ameipongeza Malawi kwa kuipokea liugha ya Kiswahili Picha : Ikulu Tanzania 

Rais wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan ametoa pongezi kwa taifa jirani Malawi kwa kuikumbatia kiswahili na kuifundisha katika shule zake.

Mama Samia alikuwa akizungumza katika ziara yake ya siku tatu nchini Malawi ambapo aliwataka wananchi wa taifa hilo kujifundisha lugha hiyo zaidi kwani 'itaimarisha uhusiano wa kibiashara na majirani zao'.

''Kiswahili ndio lugha itakayosaidia kuunganisha bara la Afrika, alisema Rais Samia.

Tarehe 7 Julai, wakati dunia inaadhimisha siku ya Kiswahili duniani, Rais wa Malawi aliagiza shule zote nchini humo, kuanza kufundisha lugha ya Kiswahili kama njia ya kuimarisha uhusiano na mataifa jirani.

"Ninafuraha kuwajulisha ninyi nyote kwamba nimemshirikisha Mheshimiwa Rais Samia, kuhusu habari za kusisimua za uamuzi wa utawala wangu wa kuanzisha masomo ya lugha ya Kiswahili ili kuimarisha uhusiano na nchi dada na Malawi zinazozungumza lugha ya Kiswahili kama Tanzania," alisema Rais Chakwera. "Na wizara yangu ya elimu imeagizwa kutekeleza sera hiyo kwa haraka."

Rais Chakwera aliyasema haya katika taarifa ya pamoja na Rais Samia iliyopeperushwa kupitia televisheni ya taifa.

''Tanzania iko tayari kutoa kila kinachohitajika ili Kiswahili kifundishwe katika shule za Malawi. Tuko tayari kwa hilo,” aliongeza Rais Samia.

Kuondolewa vikwazo

Wakati wa ziara hiyo ya siku tatu nchini Malawi, Rais Samia Hassan pia aliagiza kuondolewa kwa vikwazo vya kibiashara katika mipaka ya nchi yake na Malawi.

''Pamoja na mwenzangu Rais wa Malawi, Mh. Chakwera, tumewataka mawaziri husika kukaa chini na kutafakari namna ya kuondoa vikwazo vya kibiashara ili maono ya serikali zote mbili yaweze kufikiwa.'' aliongeza Rais Samia.

Rais Samia alikuwa nchini Malawi kwa mualiko wa mwenyeji wake, kuhudhuria maadhimisho ya miaka 59 ya uhuru wa taifa hilo.

TRT Afrika