Na Lulu Sanga
Ni siku ya tatu sasa baadhi ya wafanyabiashara katika moja ya soko kubwa zaidi Afrika Mashariki Kariakoo kufanya mgomo wa kutofungua maduka yao kutokana na kero mbalimbali zinazo wakabili.
Hata hivyo hatua yao ya kufanya mgomo ilipelekea Waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa kufika katika eneo hilo siku hiyohiyo na kuwaahidi kufanyia kazi kero zao lakini pia kukutana nao siku ya jumatano kwa mazungumzo zaidi ili kupata ufumbuzi huku akiwataka wafungue maduka kazi iendelee.
Na siku moja baada ya kuzungumza na Waziri Mkuu Majaliwa, baadhi ya wafanyabiashara hao wameonyesha nia yakuendelea na kazi zao huku wengine wakibaki katika msimamo wa kutofungua maduka mpaka wazungumze na Rais juu ya changamoto zinazo wakabili.
Lakini nini hasa kiini cha vuguvugu hilo?
TRT Afrika imezungumza na Abdallah Mwinyi Katibu Mkuu mstaafu wa jumuiya ya wafanyabiashara Tanzania anabainisha maeneo kadhaa ambayo wafanyabiashara wanataka yafanyiwe kazi ikiwepo sheria ya usajili wa sehemu ya kuhifadhi bidhaa.
“Taaruki inatokana na sheria mpya ya usajili wa sehemu za kuhifadhi bidhaa ambayo ni bure lakini shida ya hii sheria kila katikati ya mwezi unapeleka hesabu ya stoo uliyosajili kila kilichoingia na kila kilichotoka”, anasema Mwinyi.
Tofauti na hilo amezungumzia sheria kali ya kodi ya forodha ambayo wafanyabiashara wanaona inatishia mitaji na haina uhalisia.
“Sheria ya forodha iliyopo yani kodi ipo juu sana haitekelezeki na ilisha lalamikiwa kwa muda mrefu na inasababisha rushwa kubwa kubwa na rushwa ndogo ndogo hasa kwa wafanyabiashara kwani faini zake hazilipiki. Viwango vya kodi pale vya forodha havitekelezeki havilipiki haviendani na uhalisia wa wafanyabiashara” anasisitiza Abdallah Mwinyi.
Pia amefafanua juu ya kamata kamata inayofanywa na kikosi cha mamlaka ya mapato kuhusu kodi.
“Usumbufu mwingine ni mamlaka ya mapato kukamata kamata watu na kutaka kodi kwani wanakamata mzigo wa risiti na kusema mzigo hauendani na bidhaa halisi hii imekua usumbufu mkubwa sana bila kujali ni kwa mgeni au mwenyeji.” Mwinyi aongeza.
Hata hivyo mfanyabiashara huyo anasema huenda njia ya mgomo iliyotumiwa na wafanyabiashara si bora lakini ni kutapatapa ilimradi waokoe mitaji yao sababu inatokana na uhalisia wa hali iliyopo.
“Inawezekana njia waliyotumia wafanyabiashara kudai haki au kutetea mahitaji yao si nzuri ila naitaka serikali iwaelewe kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitano wafanya biashara wamepitia magumu makubwa ambayo yamepelekea kuathiri biashara. Wengine wamefilisika waliopo wanahali mbaya, serikali inapaswa ielewe maumivu wanayopitia” anaongeza mfanyabiashara huyo.
Hata hivyo amesisitiza kukutana na rais si kitu chepesi anajua rais ana uwezo wa kutuma wawakilishi lakini mambo ya kodi ni mambo ya kisera yanapaswa kupitia bunge.
“Natamani ata akituma wawakilishi wake wenye nia ya dhati ya kupata suluhisho itatosha kwetu. Kwa sababu akija akasema nimeyachukua lakini vitu havibadiliki mnakua hamja tatua ila wakija wawakilishi wakatibu vidonda vyetu sisi tutakuwa sawa”, anamaliza Mwinyi.
Hata hivyo amewataka wafanyabiashara wenzie kuwa watulivu kwenye maamuzi yao huku wakiendelea kushikamana na kuwasilisha hoja zao kwa utulivu zaidi.
Serikali ya Tanzania Inasemaje?
Serikali ya Tanzania kupitia waziri mkuu wake Kassim Majaliwa amewataka wafanyabiashara wa Kariakoo kufungua maduka yao huku akiahidi kukaa meza moja siku ya Jumatano ili kupata suluhisho.
Hata hivyo Waziri Mkuu huyo amekemea malimbikizo yanayofanywa na mamlaka ya mapato Tanzania akiwataka kuacha mara moja tabia ya uonevu dhidi ya wafanyabiashara.
“Tabia ya kuonea wafanyabiashara ikome mara moja, hii ya kukusanya tu mnakusanya tu mpaka damu itoke hii sio sawa, wengine mnawazidishia kodi ili mkae nao chini muwaombe rushwa na hii rushwa inafanya wafanyabiashara watoe hadi pesa zao za mauzo” Kassim Majaliwa.
“Wafanyabiashara sikieni ombi la Serikali fungueni maduka yenu.” Waziri Mkuu Tanzania.
Hata hivyo kauli ya Waziri huyo aliyoitoa juzi jioni imefanya baadhi ya wafanyabiashara kufungua maduka yao huku wengine wakiendelea na mgomo hali iliyopelekea mapolisi kuingilia kati.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaamm, Muliro Jumanne Muliro, amesema amelazimika kufika Kariakoo na Timu yake ili kuwadhibiti baadhi ya wafanyabiashara wanaowatishia wafanyabiashara wengine wasifungue maduka.
"Kama kuna watu wanataka kuendelea na biashara na kufungua maduka yao hawapaswi kutishwa hata kidogo, kila mtu ana uhuru wa kufanya anachotaka kufanya" anasema Muliro.
"Natoa tahadhari juu ya kuingilia uhuru wa Mtu kwenye biashara zake, anayefunga afunge lakini anayefungua asitishwe wala asifanyiwe kitu chochote, hilo ndio jukumu letu Jeshi la Polisi, tunashukuru baadhi ya Mitaa maduka yanafunguliwa" amesisitiza Muliro.
Nini kinachoendelea Sasa?
Baadhi ya maduka tayari yamefunguliwa lakini wengine wanaendelea na mgomo. Hata hivyo mazungumzo baina ya waziri mkuu na wafanyabiashara hao yanatarajiwa kufanyika leo mchana
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo Martini Mbwana akiwa anazungumza na vyombo vya habari jana amesema mazungumzo yaliyofanywa na waziri mkuu siku ya jumatatu ni chanya na tayari wanasubiri kufanya kikao baadae na waziri mkuu kama alivyoahidi hapo awali ili kupata suluhisho la kudumu.
Hata hivyo amewanyooshea vidole wale wanaogoma kutii agizo la waziri mkuu la kufungua maduka kwa kusema kuwa ni kundi tu la watu wanao washawishi baadhi ya wafanyabiashara waendeleze mgomo kwa maslahi yao binafsi.
“Shida sio kwa sisi viongozi, shida ni kikundi cha watu wajanja ndio maana nimewaomba viongozi wa usalama wafanye kazi yao sababu hizi Jumuiya wengine wanapata maslahi yao binafsi kwa manufaa yao na kuonesha picha mbaya kuwa serikali haisikilizi Wafanyabiashara.” Martin Mbwana akizungumza na wanahabari.
Hata hivyo jeshi la polisi nchini humo limejidhatiti kusimamia usalama wa wote watakao amua kufungua maduka yao.