Rais wa Rwanda Paul Kagame, amewaagiza wabunge wa nchi hiyo kuhakikisha kuwa wanadhibiti makanisa na kurejesha utulivu na ustaarabu kwenye nyumba hizo za ibada.
Kagame, ambaye alikuwa akizungumza wakati wa kumuapisha Waziri Mkuu Edouard Ngirente, Agosti 14 na wabunge wapya 80, Kagame alishangazwa na idadi ya makanisa nchini humo, akisisitiza kuwa kuwa mengi yalianzishwa kwa minajili ya kuwafaidisha watu wachache.
“Ni kitu gani kimewapata ndugu zangu Wanyarwanda mdondokee kirahisi rahisi hivyo?" alihoji kiongozi huyo.
Kiongozi huyo, ametaka kuwepo msako mkali dhidi ya watu wanaowalaghai wengine ili kupata pesa zao kwa kisingizio cha imani na ikibidi waanze kulipa kodi.
“Kuna watu wanafanya fujo kwa jina la Mungu na unaogopa kuwawajibisha, ni watu kama wewe na si miungu. Unapaswa kuhoji wanachozungumza na kufanya,” alisisitiza.
Hivi karibuni, Rais Kagame aliamuru kufungwa kwa makanisa kadhaa nchini humo, huku akitaka kuwepo na udhibiti mkubwa wa nyumba za ibada.