Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imezitaka nchi wanachama kutumia njia sahihi za kutatua misuguano baina yao, huku ikiziomba kuendelea kudumisha utangamano na undugu kati yao.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Peter Mathuki inasema Sekretarieti ya EAC ambayo inaketi mjini Arusha, Tanzania itaendelea kufanya kazi kwa ukaribu na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Salva Kiir Mayardit, ambaye pia ni rais wa Sudan ya Kusini, katika kutafuta suluhu ya mizozo na misuguano yoyote inayojitokeza na itakayojitokeza miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya hiyo.
"Iwapo kutatokea mgogoro wowote kati ya nchi mbili au zaidi, Jumuiya itatumia mbinu sahihi za usuluhishi wa migogoro, ambayo kimsingi itaheshimu uhuru na tawala wa wanachama wetu," Mathuki amesema katika taarifa yake.
Ingawa taarifa hiyo haikuweka bayana, lakini kauli hii inakuja muda mfupi baada ya nchi mwanachama Burundi kufunga mipaka yake na Rwanda, huku Burundi ikimuita Rais Paul Kagame kuwa sio jirani mwema.
Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye ameituhumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa Burundi wa Red Tabara. Hii sio mara ya kwanza kwa Burundi kuelekeza tuhumu hizo kwa Rwanda, ambapo mara zote Rwanda imekuwa ikizikana tuhuma hizo.
Wakati huo huo, Rwanda imeonyesha kusikitishwa kwake na hatua ya Burundi ya kufunga mpaka, na kusema, msimamo huo utazorotesha biashara kati ya nchi mbili hizo.