Jeshi la Ulinzi nchini Rwanda (RDF) limetangaza fursa za kujiunga na jeshi la akiba la nchi hiyo.
Mchakato huo ulioanza Agosti 14, 2024 unatarajiwa kuisha Agosti 19 mwaka huu.
Kulingana na kanuni za Jeshi la Ulinzi nchini humo (RDF), askari wa akiba wanahusisha maofisa ambao wanakuwa kazini kwa muda wote na wale wa muda maalumu, lakini wanaweza kuhitajika kutoa huduma kwa jeshi hilo wakati wowote ule.
Jeshi hilo pia limesisitiza kuwa wale walio tayari kujiunga na jeshi hilo wanapaswa kuwa wahitimu wa shahada za utabibu, uhandisi na sheria pamoja na wahitimu wa shule za sekondari na vyuo vya ufundi.
Kwa mujibu wa RDF, maombo yote ya nafasi hizo yanapaswa kutumwa katika ngazi ya wilaya, huku majaribio ya waombaji yakitarajiwa kuanza Agosti 19 hadi Septemba 3.
Mara baada ya kuchaguliwa, askari hao wanatarajiwa kuhudhuria mafunzo ya miezi sita katika chuo cha mafunzo cha Gabiro, nchini Rwanda.
Kulingana na RDF, waombaji wa nafasi hizo ni lazima wawe raia wa Rwanda, wenye afya na siha njema na wenye nia dhabiti ya kujiunga na jeshi hilo.