Jeshi la Sudan linawataka vijana 'kujiunga na vita' dhidi ya vikosi hasimu

Jeshi la Sudan linawataka vijana 'kujiunga na vita' dhidi ya vikosi hasimu

Jeshi la Sudan limetoa wito kwa vijana kujiunga nao nalo katika mapambano dhidi ya vikosi hasimu vya kijeshi.
Abdel Fattah al-Burhan (katikati) anaongoza jeshi la Sudan katika kupambana na vikosi vya dharura RSF. Picha: Reuters

Jeshi la Sudan limetoa wito kwa vijana na mtu mwingine yeyote mwenye uwezo wa kupigana kujiandikisha katika makao kambi ya kijeshi iliyo karibu kwa ajili ya vita dhidi ya jeshi pinzani la RSF.

Sudan ilitumbukia katika machafuko baada ya mapigano kuzuka Aprili 15 kati ya wanajeshi, wakiongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, na Kikosi cha msaada wa dharura (RSF), kinachoongozwa na Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo.

Tangu wakati huo, zaidi ya watu 3,000 wameuawa, wizara ya afya ya nchi hiyo ilisema, wakati takriban watu milioni 2.5 wamelazimika kuyahama makazi yao, kulingana na Umoja wa Mataifa. Idadi ya kweli ya vifo inaaminika kuwa kubwa zaidi.

"Makamanda wa vitengo vya kijeshi na mikoa wameagizwa kuwapokea na kuwapa vifaa wapiganaji, na lazima wafike katika kambi ya kijeshi iliyo karibu au kitengo," jeshi lilisema Jumatatu asubuhi kwenye ukurasa wao rasmi wa Facebook.

Wito unaoendelea

Wito wa Jumatatu wa kujihami unakuja siku chache baada ya Burhan kutoa witokama huo wakati wa hotuba ya televisheni, akiwataka vijana wa Sudan na wale wanaoweza kupigana kuunga mkono jeshi, ama wakiwa katika "makazi yao au kwa kujiunga na harakati za kijeshi."

Haijabainika ikiwa wito wa Jumatatu wa kupigana silaha ulikuwa wa lazima.

Mjini Khartoum, wanajeshi wa RSF wanaonekana kuwa na nguvu katika mitaa ya jiji hilo, wakiwa wamedhibiti nyumba za raia na kuzigeuza kuwa kambi.

Katika muda wote wa mzozo huo wa wiki kumi, jeshi limejibu kwa mashambulizi ya anga ambayo yamepiga maeneo ya makazi na wakati mwingine hospitali.

Jimbo la Darfur Magharibi limeshuhudia vurugu mbaya zaidi. Katika ripoti iliyotolewa wiki mbili zilizopita na usultani wa Dar Masalit, kiongozi wa jumuiya ya kabila la Wamasalit wa Kiafrika, alishutumu wanamgambo wa RSF na Waarabu kwa "kufanya mauaji ya kimbari dhidi ya raia wa Kiafrika."

Majaribio ya kusitisha mapigano yameshindwa

Alikadiria kuwa katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, zaidi ya watu 5,000 waliuawa katika mji mkuu wa jimbo hilo, Genena.

Majaribio kadhaa ya mazungumzo ya amani yaliyoandaliwa na Riyadh na Washington katika mji wa pwani wa Saudia wa Jeddah yamevunjika, huku wapatanishi wote wawili wakiishutumu RSF na jeshi kwa kuendelea kukiuka mapatano yaliyosimamiwa na mataifa hayo mawili.

Takriban usitishaji mapigano tisa umekubaliwa tangu mzozo huo uanze, lakini hakuna uliodumu.

TRT Afrika