Na Dayo Yussuf
Sio jambo geni kuona maandamano, mabango au hata kususia hafla kubwa za michezo. Na hii ni kweli hata kwa Olimpiki.
Kama moja ya hafla kongwe zaidi za michezo ulimwenguni, takriban miaka 130, Olimpiki imejionea kampeni za kutosha za kauli kali za kisiasa ama dhidi ya hafla za michezo, siasa za kijiografia zinazohusisha nchi fulani kucheza kwenye uwanja au wanariadha wenyewe kutangaza msimamo wao juu ya matukio ya ulimwengu.
Michezo ya Olimpiki ya 2024 kwa mfano imekumbwa na hisia za kupinga kushirikishwa Israel, kupinga wanariadha wa Urusi au hata Iran na wengine wengi.
Siasa za mitaa au siasa za mipakani zinaonekana kudai nafasi kwenye jukwaa la michezo tupende au tusipende.
''Michezo ya Olimpiki inatumika kama jukwaa la watu ambao hawaonekani kusikika kupitia njia nyingine au mtu anayetafuta tu fursa nzuri ya kuvutia mamilioni ya watu ambao tayari wameusikiliza mchezo huo,'' anasema Israel Sariya, mchambuzi wa michezo na mwanzilishi wa TanzaniaSports.com.
Kwa sababu ya kile kinachoendelea ulimwenguni, haiwezekani kutenganisha watu kutoka kwa siasa au angalau kuwa na maoni.
‘’Kuna mambo mengi yanayoendelea na watu wengi wamechukua upande. Siasa za kimataifa zinawaathiri wote, kwa hivyo ni njia gani bora ya kutoa maoni yao kuliko mikusanyiko hii mikubwa? Njia bora ya kupitisha jumbe hizi ni kuwashtukiza kwa mabango na maandamano ambapo wanahakikishiwa watazamaji?’’ Anasema Sariya.

Mashirika haya ya kimataifa ya michezo yanaendeshwa kwa utaratibu.
Wana sheria zinazoongoza michezo yenyewe, wanariadha, lakini pia wapi au nani atakayeandaa.
Na hii daima huathiriwa na siasa za kijiografia au hata msimamo wa mtu binafsi juu ya wimbi la kisiasa wakati wowote.
Wataweka sheria juu ya nini cha kufanya na kutofanya wakati wa mashindano yao ambayo wote wanatarajiwa kutii.
‘’Inawezekana kuweka sheria, lakini jambo la msingi ni utamaduni wa taifa mwenyeji,’’ anasema Sariya. ‘’Kwa mfano Ufaransa ina utamaduni na imani tofauti kabisa.
Inasaidia upendeleo tofauti wa kijinsia na ujinsia, maadili ya kidini na kijamii.
''Wana wafuasi wa mrengo wa kushoto na wa kulia kabisa wa kisiasa, kwa hivyo sheria zozote utakazowawekea, nchi mwenyeji daima itasukuma ajenda zake hata ikimaanisha kuvunja sheria zako,’’ anaiambia TRT Afrika.
Kufuatia vita vinavyoendelea vya Israel huko Gaza na Urusi - Ukrain Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) ilisisitiza msimamo wake dhidi ya kuingiza siasa katika michezo kama ilivyoainishwa katika Mkataba wake.
Kwa kutambua kwamba michezo hutokea ndani ya mfumo wa jamii, mashirika ya michezo ndani ya Harakati za Olimpiki yatatumia kutoegemea upande wowote kisiasa.
IOC inasisitiza kuwa inapinga unyanyasaji wowote wa kisiasa au kibiashara wa michezo na wanariadha.
Lakini michezo ya Olimpiki ya Paris imekuwa ikizongwa na miito ya kupiga marufuku timu ya Israel kushiriki kutokana na vita vilivyofanywa na serikali yao dhidi ya Gaza na Wapalestina.
Waandaaji pia wamekabiliwa na ukosoaji mkali juu ya sera yao ya kupinga hijab kwa wanariadha wa Ufaransa ambayo Waislamu wanaona kama maneno dhidi ya Uislamu na ubaguzi dhidi ya wanawake wa Kiislamu katika mashindano hayo.
Lakini jambo la kudhihirika zaidi ni shutuma waliopata baada ya sherehe ya ufunguzi ambapo maigizo yanayodaiwa kuwa mlo wa mwisho yamekosolewa na vikundi vya kidini na makanisa kuwa ni dhihaka na kejeli kwa imani yao.
Waandalizi hao wanasisitiza kuwa hawakutaka kosa lolote kimakusudi kwa kitendo hicho ambacho wanadai kinatoa heshima kwa miungu ya kale ya Ugiriki.
Lakini siasa inapochukua nafasi ya michezo, ina athari yoyote kwa wanariadha?
'Athari kuu ni kujiondoa kwa wafadhili. Tumeona kwa mfano katika michezo ya Olimpiki inayoendelea 2024, makampuni makubwa yameondoa ufadhili wao kufuatia mabishano yanayohusu sherehe za ufunguzi,’’ anasema Sariya. ‘’Utaona kwa muda mrefu mabishano hayo yanawaathiri wanariadha mmoja mmoja kwa sababu anayemlipia awepo hakubaliani na ujumbe unaopitishwa na waandaaji wa hafla hiyo,’’ anaiambia TRT Afrika.
Changamoto iko kwenye idadi. Tukio kama vile Olimpiki linahusisha zaidi ya wanariadha 11,000, bila kuzungumza juu ya mashabiki na wafadhili.
Kwa hivyo itakuwa ngumu sana kukidhi ajenda za kisiasa za kila mtu.
‘’Kama mtu wa michezo naamini kuwa michezo haifafanuliwi kwa hafla za ufunguzi au kufunga. Kiini kikuu cha michezo ni katika roho ya ushindani ya wanariadha katika uwanja na vipaji na uwezo wao. Maonyesho ya pembeni yasiruhusiwe kuwafunika,’’ anasema Sariya.
Iwe ya kimataifa au la, michezo hayawezi kutenganishwa na matukio ya kimataifa.
Siku zote kutakuwa na mtu anayenyakua fursa ya kuficha ujumbe mmoja au mbili, iwe siasa, mabadiliko ya hali ya hewa au dini.
‘’Michezo imeainishwa katika makundi. Kuna michezo ya mtu binafsi na michezo ya timu. Ushauri wangu kwa wanariadha binafsi ni kufikiria kazi zao wenyewe. Fikiria kilichokuleta hapo kwa sababu, ukitoa taarifa binafsi, inaweza kuathiri maisha yako ya baadaye ama binafsi au kugharimu udhamini wako wa timu nzima,’’ anasema Sariya.