Na Edward Qorro
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Kiongozi huyo wa zamani, mwenye umri wa miaka 82, ameweka wazi nia yake ya kugombea Urais katika uchaguzi mkuu wa nchi hiyo utakaofanyika Mei 29, 2024.
Hata hivyo, itamlazimu Zuma kusubiria maamuzi ya Mahakama, baada ya Tume Huru ya Uchaguzi ya Afrika Kusini kusisitiza kuwa ‘JZ’ kama anavyofahamika kwamba hana sifa za kugombea tena nafasi hiyo.
Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo ilikata rufaa kwenye Mahakama ya Juu ya nchi dhidi ya uamuzi wa mahakama ya chini, uliompatia ruhusa Zuma kushiriki uchaguzi mkuu utakaofanyika mwisho wa mwezi Mei.
Aprili mwaka huu, Mahakama ya nchi hiyo ilisema mwanasiasa huyo alikuwa huru kugombea, baada ya Tume Huru ya Uchaguzi kumzuia, ikisema kuwa Katiba inamkataza mtu kushikilia ofisi ya umma ikiwa atapatikana na hatia ya uhalifu na kuhukumiwa kifungo cha zaidi ya mwaka mmoja.
Mahakama hiyo ilikuwa inachunguza tuhuma za ufisadi wa kifedha na ukaribu aliokuwa nao na familia ya Gupta wakati wa uongozi wake.
Ni dhahiri shahiri, kuwa MK kitatoa upinzani mkubwa kwa ANC, katika uchaguzi huo.
Mtoto wa nyumbani
Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wanaamini kuwa huu ndio wakati muafaka wa Zuma kuiongoza nchi hiyo kwa awamu nyingine.
Kwa mujibu wa wachambuzi hao, Zuma ameifanyia nchi hiyo mambo makubwa hivyo anastahili kupewa nafasi nyingine.
“Zuma ana nafasi kubwa katika siasa za Afrika Kusini, kwanza kwa sababu alishiriki pakubwa katika kupigania haki na uhuru wa watu weusi nchini Afrika Kusini, kwa hiyo ana ushawishi mkubwa sana kwa marika yote,” Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Msaada wa Sheria ya CiLAO, Charles Odero anaiambia TRT Afrika.
Mwaka 1963, Zuma aliingia kifungoni kutokana na mapambano yake dhidi ya ubaguzi wa rangi na baadaye kuwa mkimbizi wa kisiasa mwaka 1975.
Kulingana na Odero, raia wa Afrika Kusini bado wana imani na Zuma.
“Zuma amekuwa Rais wa nchi hiyo mpaka pale alipopata ajali ya kisiasa na kuondolewa madarakani, lakini jamii wa Afrika Kusini bado inamchukulia kama mtoto wao, kiongozi,” anaeleza.
Sio wakati muafaka
Hata hivyo, huu unaweza usiwe wakati muafaka kwa Zuma kugombea urais, bila kujali uamuzi wa mahakama.
Moses Allan Swila, ambae ni rais wa taasisi ya Marafiki wa Afrika Mashariki, inayopatikana jijini Arusha nchini Tanzania, anasema kuwa inawezekana huu ukawa si muda muafaka kwa Zuma kurusha ndoano kwenye nafasi ya Urais, kwani bado ananuka harufu ya tuhuma za rushwa.
"Bado anachunguzwa kwa rushwa na madai mengine yanayohusiana nayo, sidhani kama yeye ni mtu sahihi kuongoza Afrika Kusini kwa wakati huu," anaiambia TRT Afrika.
Tume ya Uchaguzi ya Afrika Kusini imesema kwamba mwanasiasa huyo aliyechafuliwa na ufisadi anafaa kuzuiwa kushiriki kinyang'anyiro hicho kwani alidharau uamuzi wa mahakama, mwaka 2021.
Hata hivyo, Waafrika Kusini watalazimika kusubiri uamuzi wa Mahakama ya Kikatiba ili kujua mbichi na mbivu kuhusu kesi hiyo, ambayo wataalamu wanasema inaweza kuchukua siku kadhaa. Wakati hayo yakijiri, muda nao unayoyoma kuelekea uchaguzi mkuu wa Mei, 29.