Kulingana na ripoti hiyo, vijana wengi wa Afrika wanaonekana kuridhika na maisha./Picha: Reuters

Umoja wa Mataifa umetoa ripoti ya nchi zenye furaha zaidi duniani, wakati ulimwengu ukiwa unaadhimisha siku ya kimataifa ya furaha, Machi 20.

Katika ripoti hiyo iliyotolewa siku ya Jumatano, Libya ndiye kinara wa furaha zaidi Afrika.

Nchi hiyo ilifuatiwa na Mauritius na Afrika Kusini, wakati Lesotho ilikuwa ya mwisho kwa kuwa na furaha, kwa upande wa bara la Afrika.

Finland ilishika nafasi ya kwanza ikifuatiwa kwa karibu na Denmark, Iceland na Sweden, wakati nchi nane kutoka Afrika ziliambulia nafasi kumi za mwisho katika orodha hiyo.

Maisha bora zaidi

Raia kutoka nchi 143 duniani waliombwa kutoa tathmini ya maisha yao kutoka kiwango cha 0 mpaka 10, huku 10 ikiwakilisha maisha bora.

Matokeo kutoka miaka mitatu yametengezewa wastani na hatimaye kuwepo na orodha hiyo.

Jambo la kufurahisha zaidi ni kuona namna vijana wengi, haswa kutoka ukanda wa kusini mwa jangwa la Sahara wakiridhika na maisha, ingawa hali ya maisha yao ilikuwa ya chini.

Ripoti hiyo, ambayo hutolewa kila mwaka, ilianzishwa mwaka 2012 na Umoja wa Mataifa, kupitia malengo endelevu ya maendeleo.

Nchi 10 za Afrika zenye furaha zaidi kulingana na ripoti hiyo

  • 66 - Libya
  • 70 - Mauritius
  • 83 - Afrika Kusini
  • 85 - Algeria
  • 89 - Congo Brazzaville (Jamhuri ya Congo)
  • 90 - Msumbiji
  • 95 -Gabon
  • 96 - Ivory Coast
  • 97 - Guinea
  • 99 - Senegal

Nchi zingine za Afrika :

  • 102 - Nigeria
  • 104 - Cameroon
  • 107 - Morocco
  • 109 - Niger
  • 110 - Burkina Faso
  • 114 - Kenya
  • 120 - Ghana
  • 127 - Egypt
  • 130 - Ethiopia

Nchi 10 zisizo na furaha:

  • 131 - Tanzania
  • 132 - Visiwa vya Komoro
  • 134 - Zambia
  • 135 - Eswatini
  • 136 - Malawi
  • 137 - Botswana
  • 138 - Zimbabwe
  • 139 - Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
  • 140 - Sierra Leone
  • 141 - Lesotho

Ripoti hiyo pia imetumia vigezo mbali mbali vikiwemo kipato, afya, ukarimu, kukosekana kwa rushwa na msaada wa kijamii.

TRT Afrika